Mgombea urais
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ali Mayay akizungumza na waandishi
wa habari akinadi sera zake za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa
TFF utakaofanyika Agosti 12, mkoani Dodoma, Kushoto ni mshambuliaji
nyota wa zamani wa Klabu ya Simba, Zamoyoni Mogella
Na Karama Kenyunko Globu ya jamii.
Mgombea urais wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Ali Mayay amesema kuwa katika uongozi wake
atahakikisha dira ya mpira wa miguu inarejea katika mstari na
kuiwezesha nchi kupata maendeleo makubwa katika sekta hiyo.
Mayay amesema hayo leo alipokuwa
ananadi sera zake katika siku ya kwanza ya uzinduzi wa kampeni kuelekea
uchaguzi mkuu wa TFF utakaofanyika Agosti 12, mkoani Dodoma. Amesema
kuwa kwa sasa hakuna dira ya mpira wa miguu na ndio chanzo cha kuwa na
maendeleo duni ya mpira kulinganisha na nchi zingine ambayo kwa sasa
zinafaidi matunda baada ya kuanzisha na kutekeleza dira hiyo.
“Kwa sasa wachezaji wengi wa
Zambia wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi, timu yao Taifa inafanya
vizuri, Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji, lakini hakuna dira na
kusababisha wao pia kukosa dira katika fani yao,” alisema Mayay.
Alisema kuwa akiwa kama
mchezaji, ameweza kuona changamoto mbalimbali za mpira wa miguu na
kuamua kugombea nafasi iliyo ili kuzitatua na lengo lingine ni kujenga
taasisi imara kwa kutumia rasilimali zilizopo kwani tatizo si vipaji,
bali ni aina gani ya uongozi unaosimamia mpira wa miguu.
Wachezaji mbalimbali waliong’aa
katika medani ya soka hapa nchini, wamepigia chapuo mchezaji wa zamani
wa timu ya Taifa, Taifa Stars Ali Mayay kuchaguliwa katika nafasi ya
urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mgombea huyo ambaye ni chaguo la
wachezaji wa zamani nchini aliungwa mkono na mshambuliaji nyota wa
zamani wa Klabu ya Simba, Zamoyoni Mogella ambaye alisema TFF inahitaji
mtu kama Mayay anayejua matatizo ya mpira wa miguu kwani ameucheza huo
mpira.
Mogella ambaye enzi zake
alipewa jina la “Golden Boy” na “Morgan” alisema kuwa wanahitaji
kuurudisha mpira kwa wenyewe huku wakiwaomba wagombea kumchagua Mayay
kwani ni wakati wa mabadiliko kwa wadau wa soka nchini kwa kumchagua
Mayay ambaye anavigezo vyote katika masuala mbalimbali ya soka na
uongozi.
“Mayay ni dira ya soka Tanzania,
amecheza soka kuanzia shuleni, katika hatua ya vilabu mpaka timu ya
Taifa, anajua nini cha kufanya ili kuleta maendeleo ya soka nchini,”
alisema Mogella.
Mchezaji wa zamani wa Yanga
Mohamed “Adolph” Rishad naye alisema kuwa Mayay ni suluhisho sahihi kwa
maendeleo ya soka nchini na si wagombea wengine zaidi wachezaji wa
mpira wa miguu wametengwa katika soka na kukosa mwamko katika mchezo
ambao wanaupenda.
Amesema kuwa kwa sasa Tanzania
ina matokeo mabaya katika soka la kimataifa ni kukosa uongozi wenye
mapenzi ya mchezo pamoja na Tanzania kuwa na vipaji vingi vya soka.
Tags
ALLY MAYAI