Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman
Jafo akimkabidhi mshindi wa pili wa maonyesho ya nanenane kanda ya kati
ambaye ni Benki Kuu ya Tanzania.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman
Jafo akimkabidhi mshindi wa tatu wa maonyesho ya nanenane kanda ya kati
ambaye ni Jeshi la Magereza.
………………………..
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman
Jafo amezitaka halmashauri zote nchini kutekeleza jukumu lao la
kuwapelekea wakulima wa vijijini teknolojia na pembejeo bora ili
kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji mali.
Jafo ametoa rai hiyo jana wakati
wa kilele cha maonyesho ya nanenane kanda ya kati inayojumuisha mikoa ya
Singida na Dodoma ambapo alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali
yalioonyesha shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na sekta binafsi
zinazosaidia katika kukuza uchumi.
Amesema kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati”
hivyo basi halmashauri zinatakiwa kuhakikisha mazao ya wakulima na
wafugaji yanapata soko kwa kutoa elimu ya kuchakata na kufungasha bidhaa
zao katika ubora unaokubalika sokoni ili mazao hayo yawe na thamani
zaidi.
Jafo amesema halmashauri zote
zinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kutenga maeneo kwa ajili ya
uwekezaji wa viwanda na kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa na huduma zote
za msingi kama vile miundombinu ya Barabara, Umeme na Maji ili kuwavutia
wawekezaji na hivyo kumsaidia mkulima na mfugaji kufikia uchumi wa
kati.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Ole Nasha ameipongeza Benki
ya Maendeleo ya Kilimo kwa kuendelea kuwezesha shughuli za kilimo nchini
huku akitoa angalizo la kutowasahau wakulima wasio na uwezo.
Ole Nasha amesema Benki hiyo
isitoe mikopo kwa wakulima wakubwa na wenye uwezo tu bali isisahau
jukumu la kuwafikia wakulima wasio na uwezo ili waweze kupata mikopo na
kuweza kulima kisasa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Wakati huo huo Naibu waziri Jafo
ametoa Wito kwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kuamua kuufanya Mkoa wa
Dodoma hasa Viwanja vya Nzuguni kuwa Kituo cha Kudumu cha Maonesho ya
nanenane kitaifa kutokana na Kijiografia kuwa katikati na Makao Makuu ya
nchi na hivyo kuwa rahisi kwa Kanda zote nchini na hata nchi za jirani
kuja kushiriki Maonesho ya Nane Nane.
Jafo amesema hayo akiunga mkono
kauli iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Dkt.
Charles Tizeba aliyesema Serikali inafikiria kuachana na utaratibu wa
kuhamisha hamisha Maonesho ya kitaifa ya Nane Nane kwenye Kanda
mbalimbali na badala yake kuwa na kituo kimoja cha Kitaifa kama ilivyo
kwa maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanavyofanyika Dar es
Salaam pekee.
Jafo amesema Uwanja wa Nane Nane
Nzuguni unahitaji kufanyiwa uwekezaji na uendelezaji wa miundombinu yake
kama barabara, umeme na maji na kuboreshwa huduma mbalimbali na
kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mikoa ya Dodoma na Singida kuweka
mkakati wa kuendeleza miundombinu hiyo kwa kuwa baada ya uwekezaji
mkubwa uwanja huo utarejesha mapato mengi.
Ameongeza kuwa Serikali za Mikoa
ya Singida na Dodoma inaweza kufanikisha ukarabati huo kwa kushirikisha
wadau mbalimbali wakiwemo Taasisi kama Benki ya Uwekezaji TIB na Benki
ya Maendeleo ya Kilimo TADB.
Washindi wa Maonesho ya Nane Nane
Kanda ya Kati yaliyoanza tangu Agosti Mosi ni Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) lililoibuka kuwa Mshindi wa jumla wa Maonesho ya Mwaka huu,
likifuatiwa na Benki Kuu ya Tanzania ikiwa mshindi wa pili na Mshindi wa
tatu akiwa ni Jeshi la Magereza.
Tags
NANENANE 2017