Na: Judith Mhina – MAELEZO
Hakika historia imejirudia, mkoa
wa Tanga ni kati ya mikoa mashuhuri nchini Tanzania kabla ya uhuru wa
Tanganyika katika kupigania uhuru, kwa kuwa ni mkoa uliokuwa na wasomi
wengi kuliko mikoa mingine wakati huo.
Hii ilitokana na uwepo wa shule
za wamisionari wa kanisa la Anglikana (UMCA) ambalo ni la kwanza kuingia
katika Pwani ya Afrika Mashariki mwaka 1878 na waliojenga shule za
Magila na Kiwanda Muheza, Korogwe misheni, Kideleko Handeni (Shule za
Kati) na Saint Andrew Minaki Pwani (shule ya Sekondari).
Hata baada ya uhuru chini ya
Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili ya uongozi wa Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere na Rais Msataafu Ali Hassan Mwinyi, mkoa
wa Tanga ulikuwa maarufu kutokana na uwepo wa viwanda vingi, njia za
reli na Bandari yenye kina kirefu yenye uwezo wa kuingiza meli kubwa za
mizigo za Kitaifa na Kimataifa.
Viwanda ambavyo vilijengwa katika
mkoa wa Tanga ni pamoja na vya chuma, mbolea, saruji, maziwa, kamba za
katani na mazulia, amboni plastic, mbao, sabuni maarufu ya mbuni,
gardenia, foma na mafuta ya nazi.
Historia hii sasa inajirudia
katika mkoa wa Tanga baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt, John Pombe Magufuli, kupigania kwa nguvu zote Mradi wa ujenzi wa
bomba la mafuta kutoka Uganda kuja nchini Tanzania ambalo litaishia
katika kijiji cha Chongoleani.
Wananchi wote wa Tanzania wana
kila sababu ya kujivunia ujenzi wa bomba hilo la mafuta ambalo
litawapatia ajira Watanzania hususan wananchi wa mkoa wa Tanga. Pongezi
kubwa ziende kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa
juhudi zake za kuhakikisha kwamba Mradi huu unakuja Tanzania. Wananchi
wa mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kulinda
heshima ya nchi yetu kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ulinzi mkali wa
Bomba hilo kila mahali lilikopita.
Kurejea kwa mkoa wa tanga katika
ramani ya Tanzania ya viwanda umedhihirishwa na Wananchi wa Chongoleani
ambao siku ya uwekaji jiwe la msingi walikuwa wawakilishi wa Watanzania
ambao hawakupata fursa ya kwenda Tanga kumshuhudia Mheshimiwa Rais na na
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakifungua
pazia la jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa Mradi huo.
Kutokana na tukio hilo la uwekaji
wa jiwe la msingi wana Chongoleani walitoa ya moyoni kwa kuonyesha
furaha yao isiyo na kifani kupitia kwa Mwenyekiti wao wa kijiji Ndugu
Mbwana Nondo wakisema; “Kwa moyo wa dhati kabisa tunamshukuru sana Rais
wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutujali Wananchi wake kwa kutuletea
neema ya mradi huu wa bomba la mafuta”.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliongeza
kwa kusema kwamba, katika maisha yetu Wananchi wa Chongoleani hatutaweza
kumsahau Mheshimiwa Rais kwa mambo mengi anayowafanyia Watanzania na
Taifa kwa ujumla na itakuwa ni kumbukumbu kwa kizazi kijacho.
“Napenda kusisitiza kwamba
tunamuahidi Rais, kuwa wote watakaopata fursa kwenye Mradi huu wa Bomba
la Mafuta, watafanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja
mmoja na Taifa kwa ujumla”. Alihitimisha Bw Nondo.
Naye Waziri wa Afya, Ustawi wa
Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu, amewaomba wanawake wa
Mkoa wa Tanga kuchangamkia fursa zinazojitokeza, kutokana na uwepo wa
mradi wa bomba la mafuta.
Akisisitiza kuhusu ajira hizo
amesema; “Kwa wale wenye ujuzi wanaweza kupata ajira za kudumu katika
mradi, ila kwa wale ambao hawana ujuzi wachangamkie fursa nyingine kama
mama lishe ambapo mkoa unjulikana kwa kujua kupika mapishi yanayovutia
walaji wengi”
Aidha, amewaasa wakulima kuona
fursa ya kulima mazao ambayo yataliwa kwa wingi kwa watumishi
watakaoajiriwa Tanga katika mradi wa bomba la mafuta. Mfano matunda na
mbogamboga ambavyo ni sehemu ya kuimarisha lishe za watumishi hao
watakao kaa Tanga.
Mradi wa Bomba la Mafuta ni
ishara njema kwa Watanzania, Serikali na Taifa kwa ujumla maana
inaonyesha dhahiri kukosekana kwa fursa kama hii kwa miaka mingi katika
mkoa wa Tanga ni fundisho kwa Watanzania hususan Wananchi wa mkoa wa
Tanga kama waswahili wasemavyo “usichezee shilingi chooni” ikiwa na
maana shilingi ikitumbukia kuipata sio rahisi.
Kila jambo jema lina fursa zake,
nalo bomba la mafuta limekuja na neema zake, mfano wana Chongoleani
kupata barabara ya kilometa 8 inayowaunganisha na barabara kuu ya kutoka
Tanga kwenda Horohoro. Hii ina maana kubwa kwa wana chongoleani
kiuchumi, maana watakuwa na wepesi wa usafiri wa mabasi na malori.
Hivyo, bidhaa zitokazo chongoleani sasa zitaenda Tanga na nje ya mkoa wa
Tanga kwa urahisi. Mfano samaki, mazao ya chakula na mengineyo.
Wafanyabiashara wetu wachangamkie
fursa iliyojitokeza watembelee eneo husika na kudadisi kipi wanachoweza
kufanya biashara kwa ajili ya kuinua kipato chao binafsi na Taifa kwa
ujumla.
Kama tujuavyo Taifa letu liko
kwenye harakati za kuelekea katika uchumi wa viwanda, na kama ujuavyo
Tanga ni Mkoa wenye kuzalisha matunda ya aina mbalimbali na mbogamboga
kwa wingi, nazi, katani, mahindi, viazi, maharagwe, samaki, viungo kama
tangawizi, iliki, pilipili manga, mdalasini, chai na mifugo kama ngombe
mbuzi na kondoo wapo kwa makundi katika ranchi zinazotambulika na wale
wanaofugwa kiasili.
Katika suala zima la bomba la
mafuta ni muhimu mikoa yote ambapo bomba linapita kutambua na kujiandaa
kuitumia fursa zilizopo na zitakazo jitokeza katika mikoa ya; Kagera,
Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma Morogoro na Tanga. Wilaya
zitakazopitiwa na bomba hilo zipo 24 na vijiji zaidi ya 180,
vitafahamishwa kwa usahihi hapo baadaye.
Kwa kuwa Wizara ya Nishati na
Madini inahamasisha kwa pamoja na wadau mbalimbali ni vema kutumia
mafunzo hayo, kujiimarisha na kuwa sehemu ya matokeo mazuri ya bomba
husika.
Bomba la Mafuta la kutoka Hoima
Uganda mpaka Tanga Chongoleani lina urefu wa Kilometa 1445 ambapo kwa
upande wa Tanzania itakuwa na jumla ya kilometa 1115 na Uganda 330.
Aidha, Mradi utatarajia kusafirisha mapipa laki mbili na kumi na sita
elfu (216,000) kwa siku .
Kijiji cha Chongoleani ndio kituo
cha mwisho ambapo mitambo mikubwa itasimikwa katika eneo hili kwa ajili
ya kusukuma mafuta eneo la baharini ili, kuweka kwenye vyombo vya
usafirishaji kusafirisha maeneo mbalimbali duniani ambayo Uganda
watakuwa wamepata soko.
Tanzania itafaidika na mradi huu
kutokana na kodi, tozo na mrahaba wa bomba la mafuta, itakayofanywa
moja kwa moja na mradi huo. Faida nyingine ambazo, sio za moja kwa moja
ni ajira, fursa za kufanya biashara katika mikoa 8 ambayo ni Kagera,
Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro na Tanga.
Tusisahau unapopata fursa moja,
ni vema kuitumia kwa kuimarisha na kuitangaza Tanga kimataifa kwa upande
wa utalii katika machimbo ya Amboni, utalii wa samaki adimu duniani
Silikanti eneo la ufukwe wa Kigombe. Samaki huyu alikuwepo duniani miaka
6000 iliyopita, ambapo alitoweka na kugundulika kuwa yupo katika pwani
ya bahari ya hindi eneo la Kigombe Muheza Tanga.
Aidha, utalii wa milima ya
Usanbara na Nnguu Kilindi, misitu ya asili ambayo kama vile miti ya
miwati inayotengeneza nta au gundi, Tao la Mashariki misitu ya asili ya
Nguu na maporomoko ya maji katika Tao la mashariki ikiwa ni pamoja na
milima ya usambara, amani, maghamba, na nguu. Uoto wa asili na baridi
ambayo isingedhaniwa kabisa kuwepo katika milima inayoelekea bahari ya
Hindi.
Pia Hifadhi ya Taifa ya
wanyamapori ya Saadani yenye kivutio cha ngiri wanaoishi katika makazi
ya binadamu ambayo ni mbuga pekee iyopo pembezoni mwa bahari katika
Afirka mashariki, pia mbuga ya Mkomazi na mbuga ya uwindaji wanyapori ya
Nnguu, madini ya aina mbalimbali, Kasa wa pembezoni mwa ufukwe wa
bahari ya Hindi na vipepeo adimu duniani wa milima ya usambara Amani. Ni
vema kuwakarimu wageni kwa utamaduni wa asili wa Tanga kwa kuwaonyesha
mapishi na ukarimu uliotukuka wa Watanzania wapatapo wageni.
Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.
Tags
HISTORIA