Aidha alisema kwamba kumekuwepo na
tafiti zinazoonesha kwamba kilimo kimekwama katika uasili wake na
kuhitajika tafiti za kuona namna bora ya kukikwamua. Hata hivyo alisema
profesa huyo, kumekuwepo na mabadiliko ya maana katika uchumi wa
vijijini, hasa kwa kuangalia uhalisia wa uchumi kwa kuzingatia fursa za
kiuchumi na masoko katika maisha ya wanakijiji.
Alisema kutokana na mabadiliko
hayo ni dhahiri kusema kwamba wakulima hawabadiliki ni kushindwa kwa
wataalamu ambao ndio walibuni na kupanga mipango ambayo haikuweza
kuwanufaisha wakulima.
Profesa Brian Van Arkadie ambaye
pia alishawahi kuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es salaam na miongoni
mwa watafiti ESRF anasema kuna hatua mbalimbali zilizofikiwa na wakulima
wa Tanzania tangu uhuru na kwamba kuna uhusiano kati ya kilimo na
maendeleo yaliyopo sasa.
Alisema katika mkutano huo wa
hadhara ulilenga kuchambua masuala muhimu yanayojitokeza katika kilimo
cha Tanzania na kuona namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo kwa
maendeleo ya taifa, kuwa kuanzia miaka ya 1970 mazao kwa ajili ya masoko
ya nje yaliporomoka sana na kusababisha taifa kutafuta njia nyingine ya
kurekebisha hali hiyo ikiwamo kuanzishwa kwa mradi wa kubadili kilimo
wa SAGCOT.
Ingawa mazao hayo ya kilimo
yameonakana kuporomoka kutoka miaka hiyo, kumekuwepo na ongezeko kubwa
la pengo la kipato kati ya watu wa mijini na vijijini huku ukuaji wa
vijijini ukikumbwa na udumavu. Pamoja na ukweli huo amesema profesa
huyo, kuna mabadiliko ya kutosha katika maeneo ya vijijini na katika
kilimo kwamba kusema hakuna maendeleo si kitu sahihi.
Alisema zipo sababu za kupungua
kwa uzalishaji wa mazao makuu kama kahawa, tumbaku, mkonge na hilo
linatokana na serikali kuingilia kati mfumo wa masoko ambao haukuwa
unaswihi. Profesa huyo alisema hata hivyo, kwa miaka 50 kilimo cha
Tanzania kimefanikiwa kulisha taifa kwa kuwezesha watu wa mijini na
vijijini kupata vyakula hasa vile vya msingi ingawa wakati mwingine
ukame ulileta usumbufu.
Huku Tanzania ikiwa na ongezeko la
watu kutoka milioni 12.3 kwa mwaka 1967 hadi milioni 44.9 kwa mwaka
2012 ni dhahiri ukuaji wa kilimo umesaidia kuiweka nchi katika hali bora
zaidi ya upatikanaji wa chakula ingawa ifikapo mwaka 2030 watu wa
mijini watakuwa wameongezeka kwa asilimia 37 na kuweka shinikizo ambalo
kwa namna nyingine linaweza kuwa na maana kwa kuwa mazao ya chakula
yatakuwa ndiyo ya biashara na hivyo kuacha kutegemea yale ya asili kama
kahawa na tumbaku.
Katika utafiti mwaka 2007,
imeonekana kwamba nusu ya mapato ya watu wa Dar es salaam yamekuwa
yakitumika kwa ajili ya kununua chakula na kufanya kiasi kikubwa cha
kazi za kilimo katika mazao ya chakula kuwa biashara nzuri kwa
wakulima.Katika mada yake profesa huyo alisititiza kwamba hakuna shaka
maendeleo nchini katika kilimo yapo lakini tafiti nyingi zimeshindwa
kuelekeza kisahihi maendeleo hayo na ukweli wa kutoneemeka kwa wakulima.
Akijadili mada hiyo ya Prof. Brian
Van Arkadie, Mtafiti mshiriki mwandamizi wa ESRF Prof Samuel Wangwe
ameshauri serikali kutonakili mikakati na sera za nchi zilizoendelea
wakati wa utekelezaji wa mikakati ya kugeuza nchi kuwa taifa la uchumi
wa kati linalotegemea viwanda.
Alisema hayo katika mhadhara
kuhusu kilimo nchini kwamba si sawa kunakili sera na mikakati ya nchi
zilizoendelea kama Uingereza, Asia ama Marekani katika kutekeleza sera
ya viwanda bali ibuni yenyewe kwa kuzingatia hali iliyopo.
Akizungumza wakati akijadili mada
iliyowasilishwa na Prof Brian Van Arkadie kutoka Uingereza kuhusu mazao
ya chakula kama ndio mazao ya biashara katika mikakati ya muda mrefu ya
kubadili kilimo cha Tanzania na athari za kisera, Prof Samuel Wangwe
alisema kila nchi ina njia yake ya kufikia ustawi na neema ya viwanda na
hivyo Tanzania lazima ifuate njia yake na sio kunakili.
“Hatuwezi kupita njia ambayo nchi
kama Uingereza, Japan, au nchi za Ulaya zimepita wakati wakikua
kiviwanda, lakini tuwe na njia yetu katika kuelekea uchumi wa viwanda .
Kama hatutakuwa makini hatutafanikiwa,” alisema.
Prof Wangwe pia alisema kwamba
mapinduzi ya Kilimo lazima yapewe kipaumbele kama taifa linataka kuwa na
uchumi wa viwanda. Akikaribisha wadau kushiriki katika mhadhara huo
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida alisema kwamba mhadhara huo
ulikuwa ni njia muafaka ya kubadilisha maarifa ili kuboresha kilimo cha
Tanzania kwa kukipatia kilimo hicho mkakati wa muda mrefu wa
kubadilika.
Alisema katika kuimarisha kilimo
hicho ni vyema masuala yanayogusa mazao ya chakula na yale ya kupeleka
nje na sera kuangaliwa kwani masuala hayo yana athari za muda mrefu
katika ukuaji wa kilimo.
Katika hadhira hiyo aliwataka
washiriki kuangalia kwa makini historia ya kilimo nchini, sera na kuona
athari za muda mrefu na fupi za sera zilizopo na kama kweli wataalamu
wametekeleza wajibu wao katika kutafuta suluhu ya wakulima au kuendelea
kudai kwamba wakulima hawako tayari kubadilika.
Dk. Kida alisema kwa kuangalia
historia ya kilimo Tanzania wataalamu hao watakuwa na nafasi kubwa ya
kuchangia katika kuendeleza kilimo ambacho ni msingi mkubwa wa maendeleo
ya mtu mmoja mmoja, kwani wapo asilimia 80 wakitegemea kilimo na taifa
ambalo linataka kwenda katika uchumi wa viwanda ambavyo mali ghafi
zinategemewa kutoka katika sekta ya kilimo.
Aidha alimshukuru Prof. Brain Van
Arkadie ambaye ndiye alikuwa msemaji mkuu kwa utafiti alioufanya ambao
aliuwasilisha mbele ya mkutano wa wasomi mbalimbali.
Prof. Van Arkadie ambaye ni
veteran ambaye alishawahi kushiriki katika mpango wa miaka mitano wa
kwanza wa maendeleo mwaka 1963. Na kufanyakazi katika maeneo mbalimbali
katika nchi za Afrika Mashariki na Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Tags
MIFUGO/KILIMO/UVUVI