Katika kuadhimisha maonesho hayo
ya Nane Nane yanayofanyika viwanja vya Nzuguni nje kidogo ya mji wa
Dodoma, banda la Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania-Tawa limekuwa
kivutio kikubwa kwenye maonesho hayo ambayo yameanza rasmi tarehe
1/8/2017.
Kivutio hicho kimetokana na kuleta
wanyamapori mbalimbali wakiwepo Simba, Chui, Nyati, Chatu, Nyoka
mbalimbali, Ndege mbali mbali, Fisi na Tausi. Kwa mara ya kwanza
maonesho haya ya kuleta wanyamapori hai yalikuwa yanafanywa na Idara ya
Wanyamapori. Safari hii TAWA wameamua kuongeza idadi ya wanyama ambayo
haikuwapo hapo awali. Mfano Nyati na Mamba.
Akizungumza katika maonesho hayo,
Afisa habari na Mahusiano wa TAWA Bw. Twaha Twaibu aliwaeleza Wandishi
wa Habari kuwa TAWA inashiriki kwa mara ya kwanza katika maonesho haya.
Aliendelea kusema TAWA ni Mamlaka iliyoanzishwa kwa Amri ya Serikali na
kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na.135 la tarehe 9 Mei, 2014.
Uanzishwaji wa Mamlaka hii ni utekelezaji wa kifungu cha 8 cha Sheria ya
kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Mamlaka ya Wanyamapori
imeanza kazi rasmi tarehe 1/Julai/2016. Makao Makuu yake kwa sasa yapo
mjini Morogoro.
Bw. Twaibu alielezea Wanahabari
kwa kusema Mamlaka ilianzishwa na Serikali kama chombo cha utekelezaji
wa majukumu ya Serikali kwa niaba ya Serikali chini ya uangalizi wa
Serikali na kuwa na mfumo unaonesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi
zaidi. Kama ilivyo kwa Mamlaka Serikali nyingine nchini, lengo la
kuanzishwa TAWA ni kutekeleza majukumu ya Idara ya Wanyamapori hasa ya
Usimamizi wa Wanyamapori nchini. Majukumu ya TAWA ni kusimamia shughuli
za utawala, ulinzi, usimamizi wa raslimali ya Wanyamapori katika maeneo
yote nje ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Ngorongoro.
Wandishi wa Habari walitaka
kupata kauli ya TAWA na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu ujenzi wa
mradi wa uzalishaji umeme wa Stiglers Gorge uliyoko ndani ya Pori la
Akiba Selous, kama TAWA na Wizara wanasemaje?
Bw. Twaibu aliwaeleza
wanahabari kuwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA kama
Wasimamizi Wakuu wa Pori la Akiba Selous (Urithi wa Dunia) wanaunga
mkono maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuri kujenga mradi
mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika Mto Rufiji kwenye Pori la Akiba la
Selous ambao ukikamilika unatarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 2,100.
Aidha Bw.Twaibu akiwa kama
mhifadhi na mtu wa habari amesisitiza kuwa ujenzi wa mradi huo hauna
tafsiri kwamba Tanzania haithamini masuala ya uhifadhi bali unazingatia
uhifadhi wenye manufaa kwa jamii na maendeleo ya taifa na hasa dhamira
ya Serikali ya rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuelekea Tanzania ya
Viwanda ambayo inahitaji nishati ya umeme itakayotosheleza mahitaji ya
Taifa.
Twaibu amesema Tanzania inatambua
umuhimu wa uhifadhi ndiyo maana imetenga eneo la zaidi ya asilimia 28 ya
eneo lote la nchi kavu Tanzania bara kwaajili ya uhifadhi wa aina
mbalimbali ukiwemo wa wanyamapori na misitu ya vyanzo vya maji ambayo ni
muhimu kwa shughuli za kijamii na kiuchumi “ni nchi chache sana duniani
zenye eneo kubwa la uhifadhi kama Tanzania,” alisisitiza Twaibu.
Ametoa mfano wa nchi ya Qatar
ambayo amesema ilikuwa na eneo la uhifadhi lililokuwa kwenye orodha ya
maeneo ya Urithi wa Dunia) kutokana na uwepo wa baadhi ya viumbe adimu
lakini walipogundua mafuta, waliamua kujitoa kwenye urithi wa dunia ili
wachimbe mafuta na kuinufaisha nchi hiyo na maendeleo ya wananchi wake.
Alipoulizwa kuhusu TAWA
inakabiliana vipi au inasemaje kuingiza mifugo kwenye Maeneo ya Mapori
ya Akiba na Tengefu. Bw. Twaibu alisema tatizo la mifugo kwenye maeneo
yaliyohifadhiwa TAWA inatekeleza Sheria Na.5 ya Mwaka 2009 ya
Wanyamapori kutoruhusu kuingiza mifugo kwenye maeneo ya Hifadhi. TAWA
kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na Mahakama inasimamia
Sheria hii iliyotungwa na Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania
ambazo zinakataza mifugo kuingia hifadhini kinyume cha Sheria.
Bw. Twaibu amewaomba wananchi
kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo katika Mapori ya Akiba kwa
kutolea mfano Pori la Akiba Selous ambalo ndilo pori kubwa kuliko yote
Barani Afrika lenye ukubwa wa eneo za mraba zaidi ya 50,000. Kuna
vivutio vya utalii na wanyamapori mbalimbali wakiwemo Tembo wakubwa
kuliko wote hapa nchini, kuna Nyati, Twiga, Viboko, Swala, na Ndege
mbalimbali linasimamiwa na TAWA.
Twaibu amewaomba pia wananchi wa
Dodoma pia wanaweza kutembelea pori la Akiba ambalo lipo ndani ya Mkoa
wa Dodoma pori la Akiba Swagaswaga katika wilaya za Kondoa, Singida
Vijijini na Chemba kuna wanyama mbalimbali.
Na mwisho amewaomba wananchi wote
wa Dodoma waje kutembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii
kujionea vivutio mbalimbali vya utalii wakiwepo wanyampori hai, ambao
watapewa maelezo ya kutembelea maeneo wanakoishi na jinsi ya kufika
maeneo hayo kama utalii wa ndani.
Tags
NANENANE 2017