Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amempongeza Mwenyekiti mpya wa Bodi
ya Ligi Kuu, Clement Andrew Sanga wa Young Africans kwa kuchaguliwa kuwa
Mwenyekiti mpya wa TPLB baada ya kupata kura 10 kati ya 16.
Katika katika uchaguzi
uliofanyika leo Oktoba 15, 2017 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, Mpinzani wa Sanga, Hamad Yahya Juma wa Mtibwa Sugar alipata
kura sita kati ya 16 za Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Wakati Sanga akichaguliwa kuwa
Mwenyekiti, Shani Christoms Mligo wa Azam FC alichaguliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti wa TPLB. Shani aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo alipata
kura 15 kati ya 16 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Nafasi tatu za kuwakilisha klabu
za Ligi Kuu kwenye Kamati ya Uongozi zilivutia wagombea wawili; Hamisi
Mshuda Madaki (Kagera Sugar) na Ramadhani Marco Mahano (Lipuli) ambao
wote wameshinda. Madaki alipata kura 12 na Mahano 13.
Almasi Jumapili Kasongo kutoka
Ashanti United FC ni mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi ya
uwakilishi wa klabu za Ligi Daraja la Kwanza. Alishinda nafasi hiyo kwa
kupata kura 35 kati ya 40 zilizopigwa.
Edgar William Chibura kutoka
Abajalo FC alishinda nafasi ya Ujumbe kutoka Klabu za Ligi Daraja la
Pili ambako zina nafasi moja kwenye Kamati ya Uongozi ya TPLB. Chibura
alipata kura 35 kati ya 40.
“Natuma salamu zangu za pongezi
kwa wote walioshinda. Nina imani nao kwamba tutashirikiana vema, kufanya
kazi katika sekta ya mpira wa miguu, najua wanajua changamoto za ligi
yetu hivyo naamini wataweza,” amesema Rais Karia mara baada ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Revocatus Kuuli
kutangaza matokeo.
Mapema kabisa leo asubuhi, Rais
Karia aliahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati mpya ya Uongozi
wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) waliochaguliwa leo Oktoba 15, 2017.
Rais Karia aliyeambatana na Makamu
wa Rais wa TFF, Michael Wambura pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF,
Kidao Wilfred alitoa ahadi hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza
la TPLB uliofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
“Tupo kwenye kikao hiki ambacho
pia kitachagua viongozi wakaoongoza miaka minne ijayo, viongozi
watakaochaguliwa leo kwa nia njema wataongoza Bodi kwa miaka minne…
“Bahati nzuri nilikuwa mmoja wa
viongozi wa kwanza wa Bodi ya Ligi. Kwa hiyo najua changamoto tangu
uundwaji wake. Hivyo nakifahamu chombo hiki vema, najua kwa undani
malengo ya chombo hiki, lazima tuyafikie.
“…Lakini niwahakikishie tu kwamba
hatutafika kama tutaendesha shughuli zetu bila uwazi, uadilifu na
uwajibikaji,” amesema Rais Karia.
“Naahidi kuona kamba chombo hiki
kipo huru. TFF itakuwa ikifanya monitoring. Tukiona mambo hayaendi sawa,
hatutasita kukaa nanyi watu wa Bodi ili tushirikiane kuweka mambo
sawa, mvumiliane huku mkifuata taratibu,” amesema.
Rais Karia amesema kwamba
uadilifu, uwazi na uwajibikaji upo zaidi kwa lengo la mpira wa miguu
kuchezwa kwa weledi ili tupate mabingwa wa kweli katika mashindano
yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.
Rais Karia aliasa viongozi wa klabu kubadilika na hasa kutoa ushirikiano kwa viongozi wa TPLB, “Nami nitatoa ushirikiano kwenu.”
Awali kabisa Mwenyekiti wa TPLB,
Hamad Yahya akimkaribisha Rais Karia, aliwakaribisha viongozi wote
waliohudhuria huku akiwapa pole kwa safari ndefu hadi kuja kwenye
mkutano.
Baada ya matokeo, Yahya alirudi
tena kuzungumza na Wajumbe ambako aliwashukuru kwa ushirikiano waliompa
wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa TPLB na kuahidi, “Nipo
bado kwenye mpira tutaendelea kushirikiana. Uchaguzi umekwisha, hakuna
makundi.”
Kwa upande wake, Sanga alimshukuru
Mungu na wajumbe wote kwa uchaguzi wa amani na utulivu, ishara inayompa
nguvu kutekeleza vema majukumu yake mapya.
Tags
RAIS WA TFF KARIA