Makocha 28 wanawake kutoka vyuo
mbalimbali vya Maendeleo ya Jamii nchini leo Oktoba 17, 2017 wamehitimu
kozi fupi ya ukocha katika kozi iliyoratibiwa kwa pamoja kati ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya Karibu
Tanzania (KTO).
Kozi hiyo ya siku mbili ambayo ni
ya pili kufanyika kwa makocha hao, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume
– Makao Makuu ya TFF ilikuwa chini ya mkufunzi wa TFF, Raymond Gweba.
Akizungumza kwenye ufungaji wa
kozi hiyo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo amesema
Serikali inafahamu kuwa inatakiwa kuwekeza kwenye soka la wanawake
kuanzia upande wa vijana na ndio maana inatengeneza mazingira na sera
zitakazowezesha mafanikio hayo.
Singo amesema nchi mbalimbali
wana maendeleo makubwa katika mpira wa miguu kwa wanawake na sasa wakati
wa Tanzania kuwekeza katika upande huo kuanzia kwa watoto na makocha.
Kadhalika, Singo amewataka
wahitimu kuchukuwa mafunzo hayo kwa uzito mkubwa kwa sababu mpira wa
miguu ya ajira na elimu hiyo itaongeza kitu kikubwa kwao.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Mpira
wa la Wanawake (TWFA), Amina Karuma amesema lengo la chama chake na TFF
kuhakikisha soka linachezwa nchi nzima linaelekea kutimia.
Amewataka wahitimu hao wa kozi
hiyo fupi kuvitumia vyeti walivyovipata kuendeleza soka la wanawake na
kufanyia kazi yale yote waliyofundishwa.
Pia ameiomba Serikali kuwaunga mkono katika maendeleo ya soka la wanawake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
ufundi wa TFF Salum Madadi amesema kufundisha watoto kuna changamoto
nyingi, lakini makocha hao wamefundishwa maarifa ya jinsi ya kukabiliana
nazo.
Amesema maarifa hayo sio makocha
wote wanaweza kuyapata lakini wameona umuhimu mkubwa kwa wahitimu hao
kuweza kuyapata ili kwenda kuibua vipaji kuanzia chini.
Wahitimu wa kozi hiyo wamepatiwa vyeti vya ushiriki na vifaa vya michezo ikiwemo koni na mipira.
Tags
UKOCHA WANAWAKE