Mkuu wa jeshi la Polisi nchini, (IGP)Simon Sirro akiwapa hamasa baadhi ya askari wa kikosi cha kuzuia fujo (FFU)mkoani Pwani katika ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani hapo.
………………………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa jeshi la
polisi nchini (IGP)Simon Sirro amewahakikishia wananchi mkoani Pwani
kuwa silaha zote zilizochukuliwa na wahalifu wa ovyo ovyo huko Kibiti na
Mkuranga zimerudi zote mkononi mwa dola na kusambaratisha mtandao wa
kiuhalifu .
Aidha ametoa rai kwa
wazazi na walimu kutoa taarifa kwenye vituo vya polisi mara
watakapobaini kuna mwanafunzi mtoro ama hajaripoti shule kwa miezi
kadhaa kwani wapo baadhi ya watoto wanaotumika kufundishwa uhalifu hata
wakutumia silaha na watu wasiowema.
Pamoja na hayo IGP
Sirro ,amesema vyombo vya ulinzi na usalama nchini vinashirikiana na
nchi ya Msumbiji kupambana na wahalifu waliobainika kukimbilia nchini
humo wakitokea Tanzania.
Aliyasema hayo
wilayani Kibaha ,mkoani Pwani ,katika ziara yake ya kikazi ya siku moja
ambapo pia alizungumza na viongozi wa mashirika ya umma,wazee maarufu
,wastaafu mbalimbali na kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapo.
IGP Sirro alieleza
kuwa ,vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kupambana na yeyote
atakaekuja kwa moto nae wataenda nae kwa moto na atakaekuja baridi
wataenda nae baridi.
Alisema serikali imeshinda kwa hilo na hali kwa sasa ni shwari katika wilaya hizo.
IGP Sirro alieleza
amepatiwa taarifa ya wanafunzi zaidi ya 1,300 mkoani hapo kuwa ni watoro
na hawajulikani walipo hivyo wazazi washirikiane kusaidia jeshi la
polisi kujua walipo.
“Kuna baadhi
misikiti,makanisa yanadaiwa yanayotumia watoto hawa katika masuala ya
kiuhalifu hivyo kuna kila sababu ya kuingia ndani kutafuta suluhu “
“Ni kazi yetu wazazi
jamii na walimu kushirikiana ,na hapa ni muhimu wazazi wasaidie kusema
watoto wao walipo ili kuwa na usalama” alisema .
Katika hatua nyingine IGP Sirro alielezea viongozi wa dini wana nafasi ya kuhakikisha wanatumia eneo lao kuhubiri amani .
“Tusidharau taarifa
hata kama ni ndogo ,tusibweteke umoja ni nguvu tusaidiane kukomesha
vitendo vya uvunjifu wa amani ” alifafanua IGP Sirro.
Akizungumzia
changamoto ya wahamiaji haramu alisema wanashirikiana na uhamiaji
kuusaka mtandao unaohusika kufanya biashara ya kusafirisha wahamiaji
haramu .
IGP Sirro alisema
hawatamvumilia yeyote anaekumbatia wahamiaji haramu kwani ni chanzo cha
kusababisha kuleta magaidi na kusafirisha bidhaa za haramu .
Alisema kwasasa wamejipanga kutaifisha mali za wafanyabiashara hao wa wahamiaji haramu na usafiri utaotumika kuwasafirisha.
Nae mkuu Wa Mkoa Wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,ameshukuru kuwepo Kwa kanda maalum kwani imeweza kuleta mafanikio makubwa .
Alisema kipindi cha
nyuma kulikuwa na hali ya sintofahamu ,watu walisitiza shughuli zao za
maendeleo ,biashara zilikwama,watu na baadhi ya viongozi walihama nyumba
zao na wengine kulala saa 12 jioni kwa kuhofia mauaji.
Mhandisi Ndikilo alieleza sasa Kibiti na Rufiji hali ni shwarii kutokana na kuimarishwa ulinzi.
Aliwataka pia
wawekezaji na wadau mbalimbali mkoani Pwani ,kujitokeza kushirikiana
kusaidia kutatua changamoto zinazolikabili jeshi la polisi ikiwemo uhaba
wa vitendea kazi ,usafiri na kujenga vituo vya polisi .
Mhandisi Ndikilo,
alisema kuwa Mkoa huo umesheheni viwanda vya kutosha hivyo ni vyema
kusaidia mambo hayo kwa manufaa ya wote wakati kukitokea uhalifu.
“Tukikumbwa na
uhalifu tunapigia simu polisi, tusiwe Wa kwanza kulaumu wakati wa
matatizo ,tukumbuke na kuwasaidia ili kufanikisha kazi zao kifanisi.;:”
alisema mkuu huyo wa mkoa .
Kwa upande wake
kamanda wa polisi mkoani Pwani ,(ACP)Jonathan Shanna alisema ziara hiyo
ni neema kwao na wamepewa maagizo mbalimbali ambayo watayafanyia kazi.
Kamanda Shanna alisema wamemfikishia kero IGP zinazowagusa askari polisi ikiwemo upungufu wa makazi .
Tags
IGP SIRRO