Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony
Mtaka akizungumza na viongozi wa Serikali, wanafunzi walioondolewa
shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na wazazi wao(hawapo
pichani) katika Shule ya Sekondari Nkoma Wilayani Itilima.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Nkoma Wilayani Itilima pamoja na wazazi wao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao maalum
kilichofanyika shuleni hapo jana.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Nkoma Wilayani Itilima pamoja na wazazi wao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao maalum
kilichofanyika shuleni hapo jana.
Mbunge wa Jimbo la Itilima
Mhe.Njalu Silanga akichangia hoja katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu kwa lengo la kuzungumza na viongozi wa Serikali,
wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na
wazazi wao wilayani Itilima.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima,
Mhe.Benson Kilangi akifuatilia kwa makini hoja mbalimbali zilizokuwa
zikiwasilishwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa
lengo la kuzungumza na viongozi wa Serikali , wanafunzi walioondolewa
shuleni kutokana na sababu mbalimbali pamoja na wazazi wao.
Mmoja wa wanafunzi walioondolewa
shuleni kutokana na kukosa sifa za kusoma katika shule za Sekondari za
Serikali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa
Serikali juu sababu ya zilizopelekea kuondolewa kwake shuleni.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi
walioondolewa shuleni kutokana na kukosa sifa za kusoma katika shule za
Sekondari za Serikali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na viongozi
wengine wa Serikali katika kikao kilichofanyika Shule ya Sekondari Nkoma
wilayani Itilima kujadili suala hilo.
…………………
Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony
Mtaka amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani
humo kuunda timu zitakazopitia na kujiridhisha juu ya majina ya
wanafunzi 633 waliotajwa kuwa Mamluki na kuondolewa shuleni kwa kukosa
sifa za kusoma shule za sekondari za Serikali kutokana na sababu
mbalimbali.
Agizo hilo amelitoa katika
Shule ya Sekondari Nkoma wilayani ITILIMA kwenye kikao chake na
viongozi, watendaji wa Serikali na wazazi wa baadhi ya wanafunzi wa
shule hiyo walioondolewa katika mfumo wa Serikali kutokana na kutumia
majina yasiyo yao, kukosa fomu za TSM 9 , kukosa vibali vya
kukariri/kurudia kidato na vibali vya uhamisho.
Mtaka amesema timu hizo
zitakazoundwa kwa kila Wilaya zifuatilie na kujiridhisha kwa kupitia
majina yote pamoja na sababu za wanafunzi hao kuitwa Mamluki na
kuondolewa katika mfumo wa Serikali zilizoanishwa, ambapo amebainisha
kuwa watendaji wa Idara ya Elimu watakaobainika kusababisha kwa uzembe
wanafunzi hao kuondolewa shuleni watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Ameongeza kuwa Wakuu wa Wilaya kwa
kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Elimu Sekondari
waitishe vikao na wanafunzi hao na wazazi wao, ili wazungumze na
kuwaeleza hatua zitakazochukuliwa baada ya kujiridhisha, baadaye taarifa
ya kila wilaya iwasilishwe mkoani.
“Kufikia Ijumaa wakuu wote wa
Wilaya na Maafisa Elimu wawe wamekutana na wanafunzi waliopata matatizo
hayo,wazazi wao na watoto wote waitwe kutoa ushuhuda wa nini
kimesababisha wao kuitwa mamluki na kurudishwa nyumbani,
wakishajiridhisha watuletee hiyo taarifa na sisi Mkoa tutaipitia na
kutoa maelekezo; tunaweza kusema wanafunzi 633 ni mamluki kumbe umamluki
wa baadhi ya wanafunzi umesababishwa na uzembe wa Watendaji wetu.”
alisisitiza Mtaka.
Aidha baada ya kusikiliza hoja za
baadhi ya wanafunzi walioondolewa katika mfumo wa shule za Serikali
pamoja na wazazi wao shuleni Nkoma na kubaini kuwa baadhi ya sababu
zilizopelekea wanafunzi hao kuondolewa zimechangiwa na uzembe wa baadhi
ya Watendaji wa Idara ya Elimu ngazi ya Wilaya na Wakuu wa Shule Mtaka
ameagiza wanafunzi hao warudishwe shuleni mara moja.
“Kuna wanafunzi hapa Nkoma
tumewasikiliza kesi zao wapo ambao walipaswa kurudia darasa , taratibu
za upatikanaji wa kibali cha kurudia darasa kama wanafunzi pamoja na
wazazi wamefanya, lakini inaonekana kuna uzembe kati ya Wakuu wa Shule
na Idara ya Elimu Wilaya, maagizo ya Serikali ya Mkoa vibali vya
wanafunzi hao kufikia tarehe 29/11/2017 viwe vimetolewa na warudishwe
shuleni” amesema Mtaka.
Sanjari na hilo Mtaka ameagiza
wanafunzi wote wanaosoma shule za Sekondari kwa kutumia majina ya watu
wengine waondolewe katika mfumo wa shule za Sekondari za Serikali na
akatoa wito kwa wazazi wao kuwapeleka katika shule binafsi au katika
utaratibu wa utahiniwa binafsi (QT) ili wafanye mitihani kama watahiniwa
binafsi (Private Candidates).
Baadhi ya wanafunzi waliondolewa
katika mfumo wa Shule za Serikali katika Shule ya Sekondari Nkoma
Wilayani Itilima kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutumia majina ya watu
wengine wamesema wako tayari kuendelea na masomo ikiwa watapata nafasi
katika shule binafsi, ambapo wazazi wao pia wamesema wako tayari
kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi ili kuwasaidia wafikie
malengo yao.
“ Nilipata taarifa kuwa mwanangu
ameondolewa shuleni kwa sababu anatumia jina la mtu mwingine na
nimeshaanza kutafuta nafasi kwenye shule za binafsi ili aendelee na
masomo kwa sababu alikuwa anafanya vizuri darasani, kwa mfano muhula
uliopita aliongoza” alisema Sumuni Daudi mmoja wa wazazi walioshiriki
kikao na Mkuu wa Mkoa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Itilima
Njalu Silanga ameomba kuwepo na darasa maalum kwa wanafunzi
watakaobainika kuwa siyo halali waandaliwe utaratibu wa kufundishwa na
baadaye wafanye mitihani kama watahiniwa wa kujitegemea ili waweze
kutimiza ndoto zao.
Tags
ELIMU