Mchg.
Pascal Mande wa Kanisa la TAG Msasani akihubiri wakati wa tamasha la
Mkesha (Campus Night 2017) wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka
mkoa wa Dodoma lilifanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga, UDOM, mwishoni mwa
wiki. (Picha na Irene Bwire)
Mwanamuziki
wa nyimbo za injili, Angel Benard na waimbaji wake, wakitumbuiza wakati
wa tamasha la Mkesha (Campus Night 2017) wa wanafunzi wa vyuo vya elimu
ya juu kutoka mkoa wa Dodoma lililofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga,
UDOM, mwishoni mwa wiki. (Picha na Irene Bwire)
Wanafunzi
wa vyuo vya elimu ya juu kutoka mkoa wa Dodoma wakifuatilia burudani
wakati wa tamasha la Mkesha (Campus Night 2017) lililofanyika kwenye
ukumbi wa Chimwaga, UDOM, mwishoni mwa wiki. (Picha na Irene Bwire)
………………………………………………………………………….
*Ataka vijana waweke malengo maishani mwao
NAIBU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Bw.
Anthony Mavunde amesema Taifa lenye maadili ndilo linaloishi na watu
wanapokosa maadili Taifa linakufa.
Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati
akiwahutubia vijana zaidi 3,500 wanaosoma vyuo vya elimu ya juu vya
mkoa wa Dodoma ambao walishiriki mkesha wa kusifu na kuabudu (Campus
Night 2017) kwenye ukumbi wa Chimwaga, mjini Dodoma.
“Naendelea
kuiona Tanzania yenye ustawi mkubwa sana kama tutakuwa na vijana wenye
kumjua Mungu, wenye hofu ya Mungu na wenye kufuata maadili mema kwani
kukosa maadili kunaua Taifa,” alisema Naibu Waziri huyo ambaye alikuwa
mgeni rasmi.
Aliwataka
vijana hao watambue kuwa wameletwa vyuoni kusoma na siyo kujihusisha na
mambo ambayo ni kinyume na maadili. “Katika maisha lazima utambue njia
yako, usipoijua utapata shida tu. Ukiifahamu njia yako ni lazima
unaitunza hadi ikufikishe mwisho,” aliongeza.
Akitoa
mfano, Naibu Waziri Mavunde aliwaeleza wanavyuo kwamba hakuna jambo
baya kama mtu kufikia hatua ya kuingia chuo kikuu au chuo kingine cha
elimu ya juu lakini asijue anapaswa kufanya nini.
“Hakuna
jambo baya kama hivi sasa uko chuo kikuu lakini hujajua unataka kufanya
nini maishani mwako. Ni sawa na kufanya biashara ya kununua mablanketi
na kwenda kuyauza Dar es Salaam ambako kuna joto wakati wote au kuamua
kufanya biashara ya ice cream katika maeneo ya baridi kama vile Mafinga,” alisema.
Mapema, akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji
Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) ICC Dodoma, Dk.
Gerald Ole Nguyaine alisema hatma ya Taifa la Tanzania iko mikononi mwa
vijana na ndiyo maana wazazi, walimu na jamii wanawekeza kwenye maisha
yao.
Aliwaeleza
vijana hao umuhimu wa wao kutambua kusudi la Mungu kwenye maisha yao.
“Na sisi tunaamini bila uwepo wa Mungu, hamtaweza kuifikia hiyo hatma
mkiwa salama. Kuna kusudi aliloliweka Mungu katika maisha yako wewe
ambaye ni kijana, na kamwe usikubali kwenda kaburini kabla hujatimiza
hilo kusudi,” alisema.
“Mungu
ana makusudi na maisha yako na sisi ndiyo maana tunawekeza kwenye
maisha yako kwa sababu tunajua lipo kusudi maalum la Mungu kukuleta
duniani. Tunatumia muda wetu, na rasilmali za Taifa ili kuhakikisha
tunawaonyesha njia iwapasayo. Hakuna jambo litafanikiwa maishani mwako
kama hauna mahusiano mazuri na Mungu wako,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CAMPUS NIGHT DODOMA, Bw. Ibrahim Kisungwe alisema mwaka huu wamefanya tamasha la campus night kwa mwaka wa saba mfululizo na kila mwaka kumekuwa na mafanikio ya aina tofauti.
Alisema
kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Made Complete’ yaani umekamilishwa ambayo
inaendana na namba saba ambayo ni namba ya ukamilifu.
Wakati huo huo, mhubiri
aliyehudumu katika tamasha hilo, Mchg. Pascal Mande wa kanisa la TAG
Msasani aliwaeleza vijana hao kwamba wanapaswa kujitambua wao ni akina
nani na wapo vyuoni kwa kusudi gani ndipo waweze kufikia kusudi la uwepo
wao.
“Kama
huwezi kujitambua wewe ni nani, hauwezi kutimiza kusudi la Mungu.
Hauwezi kutembea kwenye maono ya Mungu kama hajakubali kukamilishwa na
Bwana Yesu,” alisema.
Tamasha
hilo lilipambwa na waimbaji mbalimbali wakiwemo Mass Choir (Dodoma),
Worship Experience (Dodoma), Angel Benard (Arusha), New Life Band
(Arusha), Enos Lazaro (Dar es Salaam) na waimbaji wengine wadogo kama
Sakina Naftari (Moshi) na Jerome Venance (Arusha).
Tags
MAADILI