
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza,
imeendelea kuwang’ang’ania viongozi na makada wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) kwa kuendeleza uchunguzi dhidi yao kuhusu tuhuma za kujihusisha na
vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa uchaguzi uliomalizika Desemba
3,2017.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale leo Alhamisi Desemba
7,2017 ameieleza MCL Digital kuwa taasisi hiyo inaendelea kukusanya
ushahidi ili kuwafikisha mahakamani au kuwaachia viongozi na makada hao
ambao hata hivyo hakuwa tayari kuwataja.
Ninachoweza kukuthibitishia ni kwamba, tunaendelea na uchunguzi;
ukikamilika tutawajulisha na hatua zingine za kisheria zitafuata,”
amesema Makale.
Desemba 2,2017 maofisa wa Takukuru wilayani Ukerewe walilikamata na
kulipekua gari la Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo
alipokuwa katika kampeni za kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi
uliofanyika Desemba 3,2017 katika uwanja wa CCM Kirumba.
Akiwahutubia wana CCM baada ya kutangazwa mshindi kwa kura 555 dhidi ya
kura 520 za mshindani wake wa karibu Saidi Mecky Sadiki, Diallo
alielezea kitendo cha gari lake kupekuliwa hakikuwa cha kiungwana kwa
sababu yeye ni muumini wa vita dhidi ya rushwa ambayo ni adui wa haki
kupitia imani na ahadi yake ya mwana CCM.
Siku ya uchaguzi, maofisa wa Takukuru waliwakamata viongozi wanne wa CCM
kutoka wilayani Ukerewe kwa tuhuma za kukutwa wakigawana Sh400,000
zikiaminika kuwa za rushwa kutoka kwa mmoja wa wagombea.
Makale alisema waliokamatwa, kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana wakati
uchunguzi ukiendelea ni Gabriel Gregory, diwani wa kata ya Bukindo na
mwenzake, Nicholaus Munyoro wa kata ya Murutunguru; Steven Mzige,
Mwenyekiti wa CCM kata ya Muriti na Katibu wa Uenezi wilayani Ukerewe,
Musa Manka.
Tags
TAKUKURU