Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony
Mavunde (wa pili kushoto) akizungumza katika mkutano na Wafanyabiashara
wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma baada ya Vibanda vyao kubomolewa
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) kupisha mradi wa ujenzi wa
Reli kisasa. Kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na
wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi. Kushoto
ni Katibu wa Wafanyabiashara hao John Banda.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (wa pili kushoto) akiteta jambo na
wafanyabiashara wakati akitoka katika eneo la Stendi ya Jamatini Mjini
Dodoma baada ya kuzungumza na wafanyabiashara waliovunjiwa vibanda vyao
kupisha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo
la Jamatini Manispaa ya Dodoma wakifuatilia mkutano wao na Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo
la Dodoma Anthony Mavunde, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne
Ngede na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi.
PICHA NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI
………..
NA RAMADHANI JUMA
OFISI YA MKURUGENZI
MANISPAA YA DODOMA
HALMASHAURI ya Manispaa ya
Dodoma inatarajia kuwapatia eneo wafanyabiashara zaidi ya 550
waliovunjiwa vibanda vyao na kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO)
katika stendi ya mabasi madogo ya Jamatini ili kupisha utekelezaji wa
mradi wa Reli ya kisasa, ili waendelee kufanya biashara zao kama
kawaida.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa,
Manispaa iko katika hatua za mwisho kuandaa eneo la Makole D-Center kwa
kuweka miundombinu muhimu ikiwemo mfumo wa maji safi na maji taka ili
wafanyabiashara hao waanze kufanya shughuli zao mara moja na katika
mazingira rafiki na salama katika eneo hilo.
Aliyasema hayo alipotembelea eneo
la Jamatini na Stendi Kuu Novemba 6 mwaka huu, akiambatana na Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira Anthony Mavunde ambaye
ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, pamoja na Naibu Meya wa Halmashauri ya
Manispaa hiyo Jumanne Ngede kwa lengo la kuwapa pole wafanyabiashara hao
na kuwajulisha hatua zilizochukuliwa na Viongozi mbalimbali katika
kuhakikisha tatizo linalowakabili linapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Aliwatoa hofu ya kuwa eneo hilo
halitakuwa na wateja wengi kama ilivyokuwa eneo la stendi ya Jamatini,
ambapo aliwaambia tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge
ametoa maelekezo kwa Manispaa na Sumatra kuhakikisha daladala zinakuwa
na ruti inayopita katika eneo hilo jipya la biashara ambapo abiria
watakuwa na kituo cha kupanda na kushuka na hivyo kuongeza mzunguko wa
wateja katika eneo hilo, na kwamba utekelezaji wa maelekezo hayo
umeshaanza kufanyiwa kazi na Sumatra.
Akizungumza na wafanyabiashara ya
usafiri wa mabasi katika Stendi Kuu ya mabasi ya mikoani, Mkurugenzi
Kunambi aliwaambia kuwa, Manispaa kwa kushauriana na uongozi wa Mkoa na
wadau kama Sumatra imepanga kuhamishia Stendi hiyo katika eneo la
Chaduru au kwenye eneo la viwanja vya Nanenane vilivyopo Kata ya Nzuguni
barabara kuu ya Dodoma-Dar es Salaam.
Alisema Manispaa itazungumza na
uongozi wa wasafirishaji ili kupata mapendekezo yao juu ya eneo rafiki
zaidi miongoni mwa maeneo hayo mawili.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
Mavunde aliwataka wote walioathiriwa na zoezi hilo la bomoabomoa wawe
watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Mamlaka na Viongozi wakifanya
juhudi za makusudi kuwatafutia maeneo rafiki kwa shughuli zao huku
Naibu Meya Ngede akiwahakikishia kuwa Baraza la Madiwani litasimamia
kikamilifu suala la upatikaaji wa maeneo hayo.
Tags
BOMOA BOMOA