Huku
dirisha dogo la usajili likifungwa jana saa saa 6:00 usiku, Yanga
imefunga na wachezaji wawili, mshambuliaji na beki mmoja wa kati.
Wachezaji
hao waliosajiliwa na Yanga ni beki raia wa DR Congo, Fistoni Kayembe na
mshambuliaji Yohana Nkomola aliyekuwa kwenye kikosi cha Kilimanjaro
Stars kilichoshiriki Kombe la Chalenji.
Yanga
imewasajili nyota hao mkataba wa miaka miwili kila mmoja kwa ajili ya
kukiimarisha kikosi chao kinachojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika
mwakani ambapo wataanza na St Louis ya Shelisheli.
Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema wao wanafanya usajili kwa mujibu wa mapendekezo ya kocha wao George Lwandamina.
Mkwasa
alisema, hawana mpango wa kuongeza mchezaji mwingine katika kipindi
hiki baada ya usajili wa Nkomola na Kayemba kumalizika, kwani ndiyo
mapendekezo ya Lwandamina.
Alisema
walikuwa na mpango wa kuwasajili washambuliaji wengine wawili kutoka
Sierra Leone na Benin ambao waliwapelekea mwaliko kwa ajili ya majaribio
ili wachukue nafasi za majeruhi, Donald Ngoma na Amissi Tambwe.
“Tunafunga
usajili wa dirisha dogo na hawa wachezaji wawili ambao ni beki Kayembe
na straika Nkomola, hatuongezi mchezaji mwingine.
“Tulitaka
kusajili mastraika wawili lakini tumesitisha mpango huo kutokana na
hali za majeruhi Ngoma na Tambwe kuwa nzuri, hivyo tumeachana na usajili
mwingine,” alisema Mkwasa.
Tags
yanga