SERIKALI imeendelea kudhibiti
ubora wa elimu nchini kwa kuvichukulia hatua vyuo na shule zinazobainika
kukiuka taratibu za utoaji wa elimu ikiwa ni pamoja na kusitisha
udahili wa wanafunzi,kusitisha program zitolewazo,kupunguza idadi ya
wanafunzi waliozidi na kufuta usajili wa taasisi husika.
Aidha katika Mwaka 2017/18
ulifanyika uhakiki katika vyuo na taasisi 458 za elimu ya ufundi ambapo
jumla ya vyuo na taasisi 59 zilibainika kuwa na mapungufu na hivyo
walitakiwa kurekebisha mapungufu hayo ndani ya kipindi cha miezi mitatu
kuanzia Februari 1 Mwaka 2018,chuo kitakachoshindwa kurekebisha
mapungufu hayo kitafutiwa usajili.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni
na Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William OleNasha
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,Zubeda Sakuru
(Chadema),lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti Maalum,Susan
Lymo,.
Katika swali hilo ambalo lilihoji
“Baadhi ya shule na vyuo nchini vinaendelea kudahili wanafunzi pamoja na
kutokidhi matakwa ya sheria mbalimbali,Je serikali inachukua hatua gani
kudhibiti vyuo na shule zinazoendelea kudahili wanafunzi huku zikiwa na
mapungufu,Je hadi sasa ni vyuo na shule ngapi zilizofutiwa usajili kwa
kutokidhi matakwa ya kisheria?”
Akifafanua katika majibu yake
OleNasha alisema kwa upande wa vyuo vikuu serikali kupitia TCU ilifanya
uhakiki wa Vyuo vyote vya Elimu ya juu nchini kati ya Ocktoba 2016 na
Januari 2017 ili kuhakiki ubora wa elimu inayotolewa vyuoni .
“Taarifa ya uhakiki inaonesha
mapungufu katika baadhi ya vyuo ,kufuatia programu hiyo TCU kwa Mwaka wa
masomo 2017/18 ilisitisha udahili wa wanafunzi wa programu za Afya na
uhandisi kwenye vyuo vitano’’alisema OleNasha na kuongeza kuwa
“Vilevile,TCU ilisitisha udahili
katika program zote kwa Mwaka wa kwanza wa vyuo 14 ,katika Mwaka huo huo
wa masomo TCU imedhibiti na kuzuia vyuo vikuu kudahili wanafunzi katika
program ambazo hazijapata ithibati zipatazo 75 katika vyuo vikuu 22’’
Tags
ELIMU