Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania(TFF) Ndugu Wallace Karia ametoa salamu za pongezi kwa
timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na ile ya
chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa kufuzu katika michezo
yao iliyochezwa jana huko DR Congo na Burundi.
Ngorongoro Heroes wamefanikiwa
kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za Africa za Vijana
chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger mwezi Novemba baada ya ushindi
wake wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90 kumalizika kwa
sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza
uliochezwa nchini Tanzania wakati Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua
ya nusu fainali ya mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka 17
inayoendelea huko Burundi.
Rais wa TFF Ndugu Karia amesema
kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni faraja kubwa kwa Tanzania na
inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea kuwekeza kwenye soka la vijana.
Amesema Vijana hao wa Ngorongoro
Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada kubwa na wanastahili
pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za mabenchi ya ufundi ya
timu hizo.
“Tumepokea matokeo ya Vijana wetu
wa Ngorongoro na Serengeti Boys kwa furaha kubwa kwasababu tumekuwa
tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ambayo yanaonekana
uwanjani kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea sifa kubwa Tanzania
kwa ujumla” alisema Karia.
Aidha Rais wa TFF Ndugu Karia
amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia maandalizi mazuri zaidi
timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali
yanayowakabili.
Amesema TFF inajivunia vijana hao
ambao wanaonesha mwanga mkubwa na amewaomba watu
mbalimbali,Taasisi,makampuni kuunga mkono jitihada za TFF na kuiga mfano
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojitokeza na kuisaidia
Ngorongoro Heroes katika safari yake ya kwenda DR Congo kwenye mchezo wa
marudiano.
Amemalizia kwa kuwashukuru wote
wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira wa Tanzania huku
akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais
John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao kwa TFF.
Tags
Soka