Mkurugenzi wa Idara za Kiufundi na
Huduma za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar Bw. Ally Idrisa Shamte akifunga mafunzo ya Wadadisi
wa Utafiti wa sekta isiyo rasmi nchini mapema leo mjini Dodoma.
Mratibu wa MKURABITA Bibi
Serapia Mgembe akiwaasa wadadisi wa utafiti wa Sekta isiyo rasmi
kutekeleza majukumu yao katika maeneo waliyopangiwa kukusanya taarifa
wakati wa Utafiti wa sekta isiyo rasmi nchini mapema leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa
MKURABITA Bw. Mujungu Masyenene akiteta jambo na mratibu wa MKURABITA
wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya Wadadisi wa Utafiti wa sekta
isiyo rasmi nchini mapema leo mjini Dodoma.
Msimamizi wa wadadisi kutoka
Zanzibar Bw. Said Mohamed Said akizungumza kwa niaba ya washiriki wa
mafunzo hayo kutoka Zanzibar mapema leo mjini Dodoma.
Mgeni rasmi katika hafla ya
kufunga mafunzo ya Wadadisi wa Utafiti wa sekta isiyo rasmi nchini
ambaye ni Mkurugenzi wa Idara za Kiufundi na Huduma za Kitakwimu kutoka
Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Ally
Idrisa Shamte akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya wadadisi hao
mapema leo mjini Dodoma.
Sehemu ya Wadadisi wakijadiliana
namna yakutumia ramani wakati wa utafiti kuhusu sekta isiyo rasmi hapa
nchini mapema leo mjini Dodoma kabla ya hafla yakufunga mafunzo hayo.
Sehemu ya Wadadisi hao
wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi Idara za
Kiufundi na Huduma za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Ally Idrisa Shamte (hayupo pichani).
(Picha zote na Frank Mvungi, MAELEZO- Dodoma
………………….
Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma
Wadadisi wa Utafiti wa Sekta isiyo
rasmi wameaswa kuepuka Vitendo vya Udanganyifu wakati wa kukusanya
taarifa zitakazofanikisha utafiti huo kwa kuwa Serikali imeweka mfumo
dhabiti wa TEHAMA utakaowezesha kuwabaini wale watakaokwenda kinyume na
taratibu za Utafiti huo.
Akizungumza wakati wa hafla ya
kufunga mafunzo wa wiki moja kwa wadadisi hao leo mjini Dodoma ,
Mkurugenzi wa Idara za Kiufundi na Huduma za Kitakwimu kutoka Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Ally Idrisa Shamte
amesema Serikali inamatumani makubwa kuwa wadadisi hao watazingatia
mafunzo waliyopewa na kuepuka vitendo vya udanganyifu vinavyoweza
kupelekea kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Niwaase washiriki wote wa mafunzo
haya kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kusababisha zoezi la utafiti huu
lisiende kama lilivyopangwa kwa kuwa mtakuwa mmekwamisha mpango wa
Serikali kupata takwimu sahihi zitakazosaidia katika kupanga mipango ya
maendeleo katika ngazi ya mikoa na Taifa” Alisisitiza Shamte.
Akifafanua Shemte amesema kuwa
mafunzo waliyopata wadadisi hao yatawawezesha kuwa na mbinu za kisasa
katika kudadisi, kutumia TEHAMA wakati wa zoezi la kukusanya taarifa
hivyo kuleta ubora unaotakiwa katika takwimu zitazopatikana.
Aliongeza kuwa utafiti huo
utasaidia kuonesha jinsi sekta isiyo rasmi inavyokuwa na hivyo serikali
inaweza kupanga mipango bora zaidi yakukuza sekta hiyo.
Kwa upande wake Mratibu wa
MKURABITA Bibi Serapia Mgembe amewataka wadadisi hao kuonesha kwa
vitendo yale waliyojifunza katika mafunzo hayo kwa kuwa Serikali
imewekeza katika utafiti huo ili kuchochea maendeleo kutokana na takwimu
zitakazopatikana.
Aliongeza kuwa utafiti huo unafanyika Tanzania Bara na Zanzibar na unawashirikisha wadadisi kutoka pande zote za Muungano.
Kwa upande wake mmoja wa
wasimamizi wa utafiti huo kutoka Zanzibar Bw. Said Mohamed Said amesema
kuwa watazingatia yale yote waliyojifunza kama nyenzo yakufanikisha
utafiti huo.
Utafiti huo utakuwa ni wa nne
kufanyika nchini baada ya ule uliofanyika mwaka 1991,1995 na 2005 ambapo
utafiti wa mwaka 1991 ulibaini kuwa asilimia 10.5 ya wananchi walikuwa
wakiendesha shughuli zao katika sekta isiyo rasmi, Aidha utafiti wa
mwaka 2005 matokeo yake yalibainisha kuwa asilimia 89 ya ardhi nchini
haikuwa rasmi na asilimia 98 ya biashara ziliendeshwa katika sekta isiyo
rasmi.
Tags
wadadisi