NA MWANDISHI WETU, KATAVI
KATAVI: Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Juma Mkomi amewataka Maafisa na Askari wa Uhifadhi waliohitimu
mafunzo ya kijeshi kuhakikisha wanalinda vivutio vya utalii vilivyopo nchini na
kuongeza kuwa Filamu maarufu ya ‘The Royal Tour’ iliyozinduliwa hivi karibuni
na Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan haitakuwa na maana kama vivutio hivyo
havitalindwa
Naibu Katibu Mkomi ameyasema hayo Ijumaa Mei 13, 2022
alipokuwa akifunga mafunzo ya kijeshi kwa Maafisa na Askari 190 kutoka
TFS, TANAPA, NCAA na TAWA katika kambi ya mafunzo ya kijeshi Mlele mkoani
Katavi.
" Filamu ile imezinduliwa kwa lengo la
kuhamasisha shughuli za utalii na Uwekezaji nchini na tangu izinduliwe kila
Mtanzania na Dunia wanafahamu Tanzania kuna nini" amesema Naibu
Katibu mkuu huyo.
Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, tangu filamu hiyo
izunduliwe inafanya vizuri Kimataifa na tayari Marekani imeoneshwa katika
vituo 300 kati ya vituo 355 vilivyoripotiwa kuonesha filamu hiyo.
Amesema mafunzo hayo yakawe chachu ya kuimarisha sekta ya
utalii na kuhakikisha Watalii wanapata huduma katika mazingira bora ili
kuendana na maono ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amewaeleza Wahitimu hao kuwa wana wajibu wa
kulinda misitu, wanyamapori, malikale na vyote ambavyo vinawavutia watalii kuja
kutembelea.
" Niwaombe Wahitimu mkatanguliza mbele uzalendo kwa
kuhifadhi na kulinda vivutio vyote vya utalii vitakavyokuwa chini yenu,
msipotoa huduma nzuri kwa watalii Filamu ya Royal Tour haitakuwa na maana
yoyote" amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Kwa upande wake Mratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Fidelis
Kapalata amesema mafunzo hayo waliyoyapata katika yanakwenda kubadili mfumo wao
kufanya kazi hususan katika kipindi hiki ambacho ujio wa watalii utakuwa mkubwa
kufuatia kuzinduliwa kwa Filamu maarufu ya Royal Tour
Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia – Utawala (SACC-Admn), Luoga
Erasto anasema ni matarajio ya Jeshi la Uhifadhi – TFS baada ya mafunzo hayo
wahitimu watakwenda kuishi utamaduni wa kijeshi na kuongeza kasi, ufanisi na
uzalendo katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa rasilimali za nchi.
“Niipongeze Wizaya ya Maliasili na Utalii kwa kuratibu
mafunzo haya yenye lengo la kubadirisha mfumo wa utendaji toka ule wa kiraia na
kuwa wakijeshi, sasa taasisi zote za Wizara zinakuwa na mfumo mmoja wa kijeshi
ambao utasaidia katika mabadiliko ya kiutendaji,” anasema SACC Luoga.
Katika mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe.
Filberto Sanga aliomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia uwezekano wa
kuwapangia kazi wilani mwake baadhi ya wahitimu kutoka kila taasisi ya uhifadhi
ili waweze kulinda maliasili zilizopo mkoani Katavi kwa kile alichodai mkoa huo
umebarikiwa vivutio vingi vya utalii na vingi vikiwa wilayani Mlele.
Mwisho






