Na Munir Shemweta na Anthony Ishengoma, WANMM MBEYA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha
wanatoa haki wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi.
Alisema, utoaji haki uko katika sura tofauti kuanzia zoezi
la utoaji hati, upatikanaji haki katika mabaraza ya ardhi na nyumba sambamba na
utoaji taarifa na uwezeshaji wananchi katika ardhi au rasilimali ardhi.
Alisema, baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi wamekuwa
miungu watu kwenye maeneo yao kuliko hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye ardhi yote iko chini ya mamlaka yake na kubainisha kuwa,
mwananchi anaweza kwenda ofisi ya ardhi kwa ajili ya kumilikishwa ardhi lakini
adha anayoipata wakati wa kuomba kupata uhalali wa kumiliki ardhi yake basi
maafisa ardhi wamekuwa wakijizungusha bila kumsaidia.
‘’kama nilivyokwisha sema yaliyopita si ndwele tugange
yajayo, uabaishaji ufike mwisho tumeelewana ndugu zangu’’ alisema
Rdhiwani.
Naibu Waziri Kikwete alieleza hayo tarehe 13 Mei 2022
alipokutana na watumishi wa Sekta ya Ardhi Mkoa wa Mbeya ambapo
alioneshwa kutoridhishwa na utendaji kazi wa baadhi ya watumishi
wasiowaadilifu.
‘’Kama kuna mtumishi anadhani kuna suala la kula kula
ovyo kwenye Wizara hii ya ardhi basi siyo kwa nyakati hizi, ndugu zangu watendaji
wenzangu naomba tuwe waadilifu katika kutenda haki kwa wananchi.’’ Alionya
Ridhiwani Kikwete Naibu Waziri Wizara ya Ardhi.
Sambamba na hilo aliwataka Maafisa Mipango miji wa Mkoa wa
Mbeya kuwa na mipango bora ya mipango miji ili jiji Mbeya lisiendelea kuwa jiji
la makazi holela.
Kwa mujibu wa Ridhiwani, ukiwa kwenye ndege unaona milima ya
mbeya imejengwa majengo kwenye ardhi isiyopimwa ambapo aliwataka Maafisa
Mipango Miji hao kutosubiri watu kuendeleza makazi holela na baadae kujitokeza
kurasimisha maeneo hayo.
‘’Acheni kusubiri wananchi wajenge alafu nyie muwafuate
kuendeleza mipango miji badala yake muwe wa kwanza kupima na kupanga miji ili
wanachi waishi kwenye makazi bora tofauti na sasa mnapowaa na kusababisha
kuaribu milima na taswira ya jiji la Mbeya’’ alisema Ridhiwani.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Ridhiwani Kikwete yuko mkoani Mbeya kwa ziara ya siku mbili ambako mbali na na
kufanya kikao na watumishi wa sekta ya ardhi ameshiriki zoezi la utoaji hati na
leseni za makazi kwa wananchi wa halmashauri ya jiji la Mbeya pamoja na wale wa
Mamlaka ya Mji mdogo wa Mbalizi.