BANDA MEDIA BLOG

No title

 


SIYO UCHAWI WA TUNGULI

 

Adeladius Makwega-DODOMA

Mlowo ni miongoni wa Miji Midogo inayokuwa kwa kasi katika mkoa wa Songwe, binafsi nilipokuwa katika eneo hilo niliwauliza wenyeji, hivi eneo hili lilianzajeanzaje?

Ndugu hawa ambao ni wapenda sana maendeleo walinijibu kuwa eneo lao awali lilikuwa makaazi ya koo ndugu chache lakini vijiji vya ujamaa vilisababisha watu wengi watolewe mashambani wahamishiwe hapo.

Ndipo kijiji cha Ujamaa Mlowo kikaanza.

Kijiji cha Ujamaa Mlowo kilikuwa na ofisi ya TANU na ofisi ya serikali ya kijiji jirani , kwa msomaji wangu fahamu kuwa mara baada ya uhuru serikali ya TANU ilipiga marufuku vyama vingi, kwa hiyo pale Mlowo ofisi ya TANU na ofisi ya Kijiji zlikuwa jirani kabisa kwa  kuwa chama na serikali zilikuwa kitu kimoja.

Mara baada ya ASP na TANU kuungana mwaka 1977 mali zote za TANU na ASP zikawa mali ya CCM, kwa hiyo ofisi ya TANU Mlowo ikawa ya CCM.

Ndugu hawa niliwauliza swali lingine, Je eneo la Mlowo liliwezaje kubadilika kutoka kijiji na kuwa Mji Mdogo ambao unabiashara nyingi?

Walijibu kuwa eneo hilo ni njia ya kwenda Tunduma ambapo ni mpaka wa Tanzania na Zambia, pia ni njia ya kwenda Malawi mpaka wa Tanzania na Malawi na isitoshe ni njia ya kwenda Kongo mpakani mwa Tanzania na Kongo.

Kwa ndugu hawa walikuwa rafiki zangu wakaniambia kwenye biashara kuna mengi, kuna mengi mwanakwetu yaani halali na haramu.

Mpaka wa Malawi huko Ileje waliniambia haufanyi vizuri lakini mpaka unaofanya vizuri ambao ni wa Tunduma lakini kuna mpaka wa Kongo wakaniambia huu una shida kwa sababu ya hali ya siasa ya Kongo.

Siasa za Kongo hali yake huwa haitabiriki.

Nikauliza kwanini? Wakanijibu kuwa pale Mlowo kuna njia inakwenda eneo linalofahamika kama Kamsamba–Momba mpaka Sumbawanga njia hiyo ina daraja linalofahamika kama Kiliamatunda. Kwa hiyo mji huo kwa jiografia yake ukawa umechangamka kwa sababu bidhaa za Kongo zinapita hapo kama za Malawi na Zambia.

Wakaniambia bidhaa za Kongo kupita Mlowo halifahamiki sana lakini zinapita, lakini zinapita mwanakwetu.

Msomaji wangu, hawa jamaa walikuwa ni rafiki zangu kwa kuwa niliwaroga kwa kitu kimoja tu wanapokuwa na jambo lao la maendeleo ninapotoa ahadi niliwapa ahadi ya kweli. Huo mwanakwetu ndiyo ulikuwa uchawi wangu na siyo uchawi wa tunguli.

Kwa hiyo mji wa Mlowo kila siku zilivyoendelea na watu wakaongezeka na mahitaji ya huduma muhimu kama zahanati, machinjio, sehemu ya kutupa takataka, soko bora na shule nyingine za msingi na sekondari yalihitajika.

Hawa jamaa walikuwa na shule mbili za sekondari mojawapo ni Mlowo ambapo ilikuwa na wanafunzi wengi mno kwa mfano kidato cha kwanza walikuwa 371 na shule nzima wanafunzi karibu 1000.

Ili kuendana na ongezeko la wanafunzi shuleni utatatuzi wa kwanza ulikuwa ni kuongeza madarasa shuleni hapo, nakumbuka wazazi wa eneo hilo chini bodi yao ya shule walijenga madarasa nane hadi kuweka bati.

Eneo hilo lilikuwa na viongozi wa CCM na CHADEMA kwa ngazi ya mitaa lakini Diwani na Mbunge walikuwa CHADEMA ambaye niliambiwa kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 mgombea wa CHADEMA alimshinda mwanasiasa maarufu na mkongwe wa mkoa wa Songwe na Mbeya Godrey Zambi huku wakiwa na mbunge wa viti maalumu CCM ambaye kidogo alikuwa bize na majukumu mengine.CCM na CHADEMA walifanya kazi pamoja bila ugomvi.

“Sikiliza mkuu sisi tunajitambua sana, kwa sababu hakuna kitu kinachoitwa CCM au CHADEMA kinachoshikika, kije hapa, kina miguu minne, kina kiwiliwili, kina mikono na kina kichwa. Chama ni dhana tu. Sisi mkuu ni ndugu wa damu lazima tushiriki maendeleo yetu. Shule hizi ni kwa ajili ya watoto na wajukuu wetu, lazima tuchangie maendeleo na serikali inapaswa kuwa na ahadi za kweli.”

Haya aliyasema mwenyekiti wa Mamraka ya Mji mdogo wa Mlowo wakati huo ndugu George Nzoa.

Walipofika hatua hiyo ya ujenzi serikali ya wilaya lazima ichangie maana inakusanya mapato kupitia ushuru. Hawa jamaa wakaomba pesa na serikali ya Wilaya na ikawapa milioni tano kuyakamilisha madarasa machache kuweka ubao, madirisha, milango, sakafu na madawati kwa awamu ya kwanza na darasa moja lifunguliwe na kiongozi wa mwenge wa uhuru mwaka 2019.

Kazi hiyo ikafanyika vizuri chini Mwalimu Mkuu mama mmoja-mwalimu Kashilika mwalimu mmoja anajituma, anajiamiani, anajitambua, ana pumzi ya kazi hiyo, ana upenda ualimu na anafanya kazi yake kwa moyo wake wote kama yupo katika mali yake binafsi. Kazi hiyo ilisimamiwa kwa msaada wa mainjia wawili injinia Mkalimoto (sasa ni marehemu) na Injini Chaula

Katika eneo la ujenzi alikuwepo Fundi Sanifu wa Halmashauri anayefahamika kwa jina la Ndonde.

Mwanakwetu siku ilifika ulikimbiza mwenge hadi hapo, alipofika kiongozi wa Mwenge wa Uhuru aliukagua mradi huo na kuuliza maswali juu ya madirisha yalivyo mbona haya makubwa na mengine madogo.?

Kwa bahati nzuri alielezwa juu ya ramani iliyotolewa na TAMISEMI ambayo ipo katika kila ofisi ya maafisa elimu wa shule za msingi na sekondari na hasa kwa maeneo ya shule zenye hali ya hewa ya baridi upande mmoja yanakuwa makubwa na upande mwingine yanakuwa madogo.

Mwanakwetu kiongozi wa mbio za mwenge huo hakuufungua mradi huu kisa ramani ya madarasa hayo, huku kila mmoja akishangazwa na kitendo hicho hata wanafunzi walikuwa wanasoma shuleni hapo sembuse wazazi wao waliochangia  nguvu na fedha.

Lakini wanafunzi hao waliyatumia madarasa hayo na sasa ninaamini wapo kidato cha nne na mwaka huu 2022 wataufanya mtihani wa kidato cha nne.

Binafsi nina imani kati ya wanafunzi 371 ndani yake wapo madaktari kadhaa, mainjini kadhaa, walimu kadhaa, polisi kadhaa, wanajeshi kadhaa, wauguzi kadhaa, wachungaji kadhaa, mapadri kadhaa na mashekhe kadhaa wa kadhaa.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru wakati huo anatambua kijiji cha Mlowo kilivyoanza na hadi wananchi wanajenga madarasa nane kwa nguvu zao wenyewe?

Je kuukataa mradi huo si kuzikataa nguvu za wananchi? Je mwananchi ambaye alichangia katika mradi huo anaweza kumuelewa kweli kiongozi wa mbio za mwenge kwa hoja ya ramani ya darasa?

Je upoo?

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

 




Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG