Wasafirishaji Waipongeza serikali kuruhusu wenye mitaji mikubwa kuingiza mafuta
Mei 11, 2022
Dar es Salaam
CHAMA cha
Wasafirishaji Tanzania (TAT-Tanzania Association of Transporters) kimempongeza
Rais Samia Hassan na Serikali kwa hatua inazochukua kukabiliana na kupanda kwa
gharama za maisha kunakotokana na wimbi la kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
TAT chenye wanachama
wasafirishaji wa mizigo na mafuta zaidi ya 200, na ambacho ndicho chama kikubwa
nchini, kimekuwa kikifuatilia kwa karibu mwenendo wa mabadiliko ya bei za
mafuta nchini na changamoto zake kwa kuwa athari zake zinakigusa moja kwa moja
kutokana na kwamba magari ya wanachama wake husafirisha kila siku bidhaa ndani
na nje ya mipaka ya Tanzania.
Msemaji wa TAT Omar
Kiponza, amesema pamoja na changamoto zote zinazowakabili Watanzania na Sekta ya Usafirishaji, TAT
kinaamini kwamba ufumbuzi wa matatizo hayo utapatikana kwa kutumia busara na
hekima inayoonyeshwa na Rais Samia na Serikali nzima.
“Pamoja na kupanda kwa
bei ya mafuta, katika siku za karibuni yamekuwapo matukio ya migomo ya madereva
na sintofahamu kadhaa ndani ya Sekta ya Usafirishaji, TAT kinaamini kwamba yote
hayo yatatatuliwa kwa kuyakabili kama Watanzania tunaopenda na kuitakia mema
nchi yetu,” alisema Kiponza.
Rais wa TAT Mohamed
Abdullah, alisema kwamba ni kweli wapo wasafirishaji wachache wenye changamoto
na pia kuna baadhi ya madereva ambao nao wana matatizo, lakini yote haya
yanaweza kumalizwa kwa kukumbuka kwamba sisi ni Watanzania, na rabsha katika
Sekta ya Usafirishaji zinaipaka matope nchi, Serikali na Watanzania wote.
“Serikali inaendelea
kushughulikia suala la bei za mafuta na haya mambo ya migomo ya madereva na
kero za baadhi ya wasafirishaji. Tuipe muda na tuwe na subira. Tunampongeza
Mama Samia na Serikali kwa hatua
inazochukua.
“Unaweza kusema haya
yanayotokea sasa ukiacha mafuta kupanda, ni mambo yasiyo ya afya kwa Sekta ya
Usafirishaji na kwa nchi yetu. Kuna baadhi ya madereva wanatumiwa. Nia ni
kudhoofisha Bandari ya Dar es Salaam, Sekta ya Usafirishaji na uchumi wa nchi yetu.
“Madereva ni ndugu
zetu, kama kuna stahili zao wapewe. Wasafirishaji wanaopindisha haki waache
mara moja na sote kwa pamoja tujihadhari na chokochoko za kutoka nje ya nchi
zenye malengo ya kutufanya tugombane wenyewe kwa wenyewe kwa faida ya watu na
biashara za nje,” alisema Mohamed Abdullah.
Wiki hii (Jumanne, Mei
10, 2022) Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati January Makamba, ilitangaza
hatua kadhaa za kukabili kupanda kwa bei za mafuta zikiwamo ruzuku ya shilingi
bilioni 100 na ruksa kwa wafanyabiashara wenye mitaji kuingiza mafuta.

