GWAJIMA ATAKA AGIZO LA BEIJING LA MIAKA 27 ILIYOPITA KUHUSU USAWA LIKAMILISHWE
Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya
Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amewataka Wajumbe
wa Kamati ya Kitaifa kukamilisha Maazimio ya Beijing ya miaka 27, tangu
Beijing iweke maazimio ya kuwa na kizazi chenye Usawa kwani ndio matamanio ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha amewata Wajumbe
wa Kamati hiyo ya Kitaifa ya kushauri na kuratibu utekelezaji wa ahadi za nchi
katika jukwaa la kizazi chenye usawa kufanya kazi kwa weledi na kuwa chachu ya
mabadiliko kuelekea kizazi chenye usawa.
Dkt. Gwajima ametoa
rai hiyo wakati akifungua kikao cha Kamati hiyo chenye lenyo la kupokea rasimu
ya mpango kazi wa utekelezaji wa ahadi hizo, kilichofanyika jijini Dodoma leo
Dkt. Gwajima amesema
Kamati ikifanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha ahadi za nchi zinatekelezwa
katika Jukwaa, utakuwa ni mwanzo wa kizazi chenye usawa na kuwa nchi ya mfano
wa kuigwa.
"Rais amedhamiria
kuhakikisha nchi inakwenda sambamba na ulimwengu na haimwachi mtu nyuma kwa
visingizio vyovyote hasa wanawake walioachwa nyuma kwa miaka mingi hali
iliyosababisha maendeleo duni kwa watoto wa kiume na wakike, hivyo tunapaswa
kuhakikisha mlolongo huo tunaumaliza ili jamii yote tuwe na kizazi cheye usawa
na kuongeza kasi ya maendeleo maradufu" alisisitiza Gwajima.
Naye Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula akizungumza katika kikao hicho amebainisha
kwamba, Kamati hiyo tangu iteuliwe imekuwa na ushirikiano mkubwa na Wizara
katika kuhakikisha matarajio ya nchi yanafikiwa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Angellah Kairuki ameishukuru Wizara kwa ushirikiano
katika kufanikisha kuwa na rasimu ya mpango kazi utakaotumiwa na Kamati hiyo
kufanya kazi yake ya kuratibu ahadi za nchi kufikia kizazi chenye usawa.
"Malengo yetu ni
kuwa na mpango mkakati unaokidhi mazingira ya nchi yetu na usiomwacha mtu
nyuma, tangu Desemba mwaka jana Kamati imeshafanya vikao vinne kwa ajili ya
kupitia rasimu ya mpango kazi huu na sasa tupo tayari kupokea" alisema
Kairuki.
Kairuki ameongeza kuwa
hatua zinazofuata ni kuwa na vikao kwa upande wa bara na Zanzibar
ambapo Kamati
itakutana na wadau wa mbalimbali kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, sekta
binafsi, vingozi wa Dini, Makundi maalum, Wasanii, Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi, TUCTA, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar, ZATUC, Vijana
na na vituo vya ubunifu.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliiteua Kamati hiyo ya Kitaifa
mnamo tarehe 16 Desemba, 2021 kwa lengo la kushauri na kuratibu utekelezaji wa
ahadi za nchi katika Jukwaa la kizazi chenye usawa, ambapo Mhe.Rais alichagua
kutekeleza eneo la pili la kuhakikisha usawa wa jinsia.
Mpango kazi huo
unaoandaliwa kwa kushirikisha wadau wa sekta zote unatarajiwa kukamilika mwezi
Juni mwaka huu ili Kamati hiyo ianze kuufanyia kazi.