MCHUNGAJI SOMMY AIPONGEZA SHULE YA NEW LIGHT
Na Mwandishi wetu, Mirerani
ASKOFU wa Kanisa la Pentekoste Tanzania Mchungaji Sommy Severua amewapongeza walimu wa New Light Pre and Primary School kwa namna wanavyotoa taaluma endelevu kwa wanafunzi wao.
Mchungaji Severua ameyasema hayo kwenye mahafali ya wanafunzi wahitimu wa darasa la saba wa shule ya awali na msingi New Light inayomilikiwa na kanisa hilo.
Amesema walimu wamejitahidi kutoa taaluma vyema kwa wanafunzi waliosoma kwneye shule hiyo kwani wengine wameendelea na elimu yao hadi vyuo vikuu vilivyopo Ulaya.
“Tunawapongeza walimu kwa kutoa taaluma bora kwa wanafunzi kwani pamoja na mazingira yote tuliyonayo Mirerani bado wanafunzi waliosoma shule hii wamefanikiwa vyema,” amesema Mchungaji Severua.
Amesema baadhi ya mafanikio ya wanafunzi waliohitimu kwenye shule hiyo ni kuwa wapo wanasoma vyuo vikuu, wengine wamehitimu vyuo vikuu na wengine wameajiriwa serikali na taasisi binafsi.
Meneja wa shule ya awali na msingi New Light, Adam Kobelo amewataka wazazi na walezi wanaowasomesha wanafunzi kwenye shule hiyo kulipa ada zao kwa wakati.
“Shughuli nyingi zinazofanyika hapa shuleni zinahitaji fedha ikiwemo mishahara ya walimu na watumishi wengine, hivyo wazazi na walezi walipe ada za masomo bila shinikizo,” amesema Kobelo.
Amesema kitendo cha kuwarudisha watoto majumbani kwa sababu ya kutokulipa ada au madeni siyo kizuri kwani makosa siyo ya mtoto ni ya wazazi na walezi hivyo walipe ada zao.
Mmoja kati ya wanafunzi wa darasa la saba waliohitimu kwenye shule hiyo Mariam Daniel Materi amewashukuru walimu kwa kuwapa elimu kuanzia awali hadi walipohitimu.
Materi amesema walisoma vizuri kwenye shule hiyo kuanzia wakiwa wadogo chekechea hadi hivi sasa wamehitimu darasa la saba na wanajiandaa mwakani 2023 kuanza kidato cha kwanza kwa elimu ya sekondari.
