DRC yazindua kituo kikubwa cha Kifedha Kinshasa kilichojengwa na kampuni ya Kituruki
Katika jitihada za kukuza uchumi wa nchi
kupitia rasimali zake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefungua majengo
ya kituo cha kifedha katika jiji lake la Kinshasa mnamo Disemba 19, 2023.
Kituo cha Kifedha cha Kinshasa
ni kitovu cha kifedha kilichoko kimkakati katika wilaya ya Gombe jijini
Kinshasa, katika eneo la magharibi mwa DRC.
Ujenzi wa jumla ya majengo 11
katika eneo la mita za mraba 165,000 ulioanza mnamo mwezi Februari mwaka 2022
umekamilika mwezi Disemba mwaka 2023. Eneo hili kubwa linakifanya kituo hiki
kuwa kituo kikubwa zaidi cha kifedha nchini humo.
Wahandishi wa Uturuki ndio
waliojenga mradi huo kwa muda mfupi. Ubunifu wa majengo hayo ya kisasa na
ujenzi wake umefanywa na kampuni ya ujenzi ya Kituruki Milvest, kampuni tanzu
ya Miller Holding.
Tangu jiwe la msingi liwekwe
mwezi Juni mwaka 2022, ni takriban mwaka mmoja na nusu umewatosha wahandishi
hao kumaliza mradi huu mkubwa nchini. Na Jumla ya wafanya kazi 3000 ikiwa
Wakongo 1500 na Waturuki 1500 wamefanya kazi kwenye ujenzi huu.
Ndoto ya Tshisekedi imetimia
Ikiwa ni moja ya ndoto za rais
Felix Tshisekedi kuijenga DRC na kuiweka katika nafasi ya kipekee si barani
Afrika tu bali hata duniani imefikiwa baada ya kufungua kituo hicho cha
kifedha.
Ujenzi huu umeigharimu DRC
takriban dola za kimarekani 290 hadi kukamilika. Kituo kitakapoanza kazi rasmi,
watu 5000 wanatarajiwa kufanya kazi ambao watahudumu raia wa DRC kwenye sekta
ya fedha.
Kuna nini hapa kwenye kituo cha kifedha?
Kituo hiki kinajumuisha
taasisi muhimu kama vile Wizara ya Fedha na Bajeti, Kurugenzi Kuu, Mkaguzi Mkuu
wa Fedha, Sekretarieti Kuu ya Fedha na Benki ya Maendeleo. Kwa ujumla kuna
taasisi 9 zinazohusiana na Wizara ya Fedha ya nchi hiyo.
Kinasimamiwa na shirika la
kibiashara la Hazina ya Uwekezaji inayomilikiwa na serikali, ambayo inasimamia
mali isiyohamishika kama vile vituo vya kifedha na mikutano.
Jengo la ofisi za kikazi lenye
ghorofa 19 ndio refu zaidi, ndani ya eneo hili pia kuna jengo la hoteli ambao
ni uwekezaji binafsi wa kampuni ya Milvest.
Katika sifa za kipekee za
kituo hiki ni kwamba ndani yake kuna ukumbi wa mikutano wa kisasa wenye uwezo
wa kupokea watu 3000 kwa wakati mmoja na kuufanya kuwa moja wa kumbi kubwa
nchini humo. Mbali na hivyo, pia kuna kumbi binafsi za mikutano midogo midogo
kwa ujumla wake zinaweza kupokea watu 10,000.
Mahusiano mazuri ya nchi mbili hizo yazaa matunda
Mnamo Februari 2022, Rais wa
Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alitembelea DRC kama sehemu ya kukuza uhusiano
kati ya Uturuki na nchi hiyo.
Wakati wa ziara yake, rais
Erdogan alitia saini mikataba kadhaa kuhusu usalama, ulinzi na miundombinu na
nchi hiyo. Moja ya mikataba hii ilihusisha kampuni ya Kituruki ya Milvest,
ambayo DRC iliifadhili awali dola milioni 290 kwa ajili ya kujenga Kituo cha
Kifedha cha Kinshasa.
Kulingana na vifungu vya
mkataba vilivyokubaliwa kati ya DRC na Uturuki, miundombinu yote yenye ubora wa
juu itakayojengwa na Milvest itakuwa mali ya DRC baada ya miaka 49 ya uongozi
wa kampuni hiyo.
Mwenyekiti wa kampuni ya
Milvest Turhan Mildon ameiambia TRT Afrika kuwa wakati wanatekeleza ujenzi wa
mradi huu moja ya changamoto kubwa walizokutana nazo ilikuwa ni usafirishaji wa
vifaa kutoka Uturuki hadi DRC.
‘‘Tulifanya uchunguzi mapema
tulijipanga vyema, na kuna vifaa ambavyo tulivihitaji badala ya kuvisafirisha
kutoka Uturuki bali tuliwekeza katika viwanda hapa na tukazalisha hapa hapa
DRC,’’ anasema Mildon.
Watu Zaidi ya 1500
walihudhuria hafla ya ufunguzi huku Wakongo wakijawa na furaha nyusoni mwao
wakionesha kufurahishwa na uzinduzi wa kituo hicho.
Mbali na raia wa wakongo,
wakiwemo Waturuki na wafanyabiashara wa kigeni waishio nchini DRC walifika
kwenye ufunguzi huo.


.png)

