Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa akizungumza na wananchi waliokuja kupata huduma kwenye Zahanati ya Chinongwe, Ruangwa Mkoani Lindi. , Desemba 29.2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
................................................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo katika kuendeleza sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya kilimo kwenye mazao ya chakula na biashara.
Amesema lengo ni kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula na kila
Mtanzania anayejishughulisha na kilimo aweze kunufaika kwa kufanya biashara na
kukuza uchumi na mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Desemba 29, 2023) alipozungumza kwa nyakati
tofauti na wananchi katika vijiji vya Litama, Chinongwe, Likwachu, Luchelegwa
na Nandanga akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa, Lindi.
Amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha
Tanzania inakuwa kimbilio la wengine wanaohitaji chakula. “Tumuunge mkono Rais
wetu kwenye mapambano yake ya kukuza sekta ya kilimo na amefanya makubwa kwenye
sekta hii ikiwemo kuagiza kutengwa maeneo maalumu ya kilimo kwa ajili ya
vijana”
Waziri Mkuu amesema licha ya Serikali kuwa na mikakati ya kuimarisha sekta
ya kilimo, pia imeendelea kuboresha sekta nyingine za afya, elimu, maji, umeme,
miundombinu na biashara ili kuhakikisha wananchi katika maeneo mbalimbali
nchini wanapata maendeleo.
‘’Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo
kwa kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo yote nchini yakiwemo na ya
wilaya ya Ruangwa.’’
Akiwa katika kijiji cha Chinongwe Waziri Mkuu alitembelea zahanati ya kijiji
hicho ambayo miundombinu yake imefanyiwa maboresho na kumuagiza Mganga Mkuu wa
Wilaya ya Ruangwa ahakikishe anamuongeza daktari mmoja ili kuboresha huduma.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Afisa Elimu wa wilaya ya Ruangwa
aakikishe anawahamisha walimu kutoka kwenye shule zenye walimu wengi na
kuwapeleka katika shule zenye upungufu ikiwemo na shule ya msingi Litama yenye
walimu wanne huku mahitaji ni walimu wanane.
Akizungumzia uboreshaji wa miundombinu,
Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongezea bajeti
TARURA nchini ambapo kwa wilaya ya Ruangwa imeongezeka kutoka shilingi bilioni
moja hadi shilingi bilioni 4.8, kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya barabara za
ndani na madaraja, hivyo amewaomba wananchi waendelee kumuunga mkono.
(mwisho)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa akikagua miundombinu kwenye Zahanati ya Chinongwe, Ruangwa Mkoani Lindi. , Desemba 29.2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa akiangalia kichomea taka kwenye Zahanati ya Chinongwe, Ruangwa Mkoani Lindi. , Desemba 29.2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Litama katika kata ya Chinongwe, Ruangwa Mkoani Lindi. , Desemba 29.2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



