Adela na Adelina, mapacha walioanza kutetea haki za watoto wakiwa wadogo
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam,
Tanzania
Adela Alex na Adelina Alex ni mabinti wawili ambao
nyuso zao siku zote zimejawa na furaha. Tabasamu pana ndilo linalopamba nyuso
zao. Kama majina yao yanavyofanana, ndivyo sura zao zinavyofanana hivyo hivyo.
Hawa ni mabinti mapacha, waliopo jijini Dar es Salaam
nchini Tanzania. Wana umri wa miaka 13, wakijiandaa kuanza kidato cha kwanza
wakati wowote kuanzia sasa.
Hata hivyo, ni miongoni mwa mabinti wachache nchini
humo ambao wameonyesha ujasiri wa kuanza kutetea haki za watoto wenzao wakiwa
na umri mdogo kabisa.
Chanzo cha harakati zao
Harakati zao zimejikita zaidi, hasa katika kutetea
haki za watoto hasa wale wanaonyanyapaliwa kutokana na sababu mbalimbali.
Msukumo wa harakati zao ulianzia mwaka 2016 baada
ya Adela kuanza kunyanyapaliwa shuleni na hata kwenye jamii yake kutokana na
tatizo la mfumo wa hewa.
"Adela anasumbuliwa na tatizo la mfumo wa hewa
ambao unasababisha mawimbi yake ya ubongo kucheza na mpaka sasa haujagundulika
jina lake. Ndio maana tuko katika utafiti kwa sababu hata dawa anazotumia, sio
zinazotibu huo ugonjwa," anasema Sara Emmanuel Kitainda, ambae ni mama
mzazi wa watoto hao.
Adela alimwambia mwandishi wa habari hii, kuwa hali
hiyo imemfanya kubandikwa majina ambayo hayapendi hasa akiwa shule, na wakati
mwengine, kulinganishwa na Adelina kwenye matokeo ya mitihani.
“Katika suala la ufaulu wa masomo, mara nyingi
nalinganishwa na mwenzangu ambae anafaulu kuniliko. Wananiambia kwamba
mwenzangu ana akili kuniliko kwa sababu mimi nacheza darasani,” anasema Adela.
Kwa sasa mabinti hawa, chini ya
usaidizi wa mama yao, wako katika hatua za mwisho za kusajili taasisi yao
itakayoitwa ‘Adela Foundation’ lengo lake ni kuongeza nguvu katika harakati
zao.
"Mara nyingi jamii inawaona watoto kama
hawajui haki zao, hivyo jukumu la kuwalinda huachiwa wazazi na walezi. Lakini
mambo yamebadilika hivi sasa, matumizi ya mitandao na teknolojia inawajengea
watoto uelewa wa kutambua haki zao mapema zaidi," anasema Sara.
Wamekuwa wakizunguka mashuleni, na kuandaa
makongamano mbalimbali ili kufikisha elimu ya kuupinga ukatili kwa watoto na
ukiukwaji wa haki za binadamu kwa ujumla.
Tangu walipoanza harakati hizo
licha ya kuwa na matokeo chanya katika baadhi ya maeneo, lakini wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto hasa kutokana na kasumba iliyoko ndani ya jamii
kwamba watoto hawawezi kuwakosoa wakubwa.
Adelina anasema mara kadhaa wamekuwa wakionekana
kama hawana adabu kutokana kuendesha harakati hizo za kudai haki na maslahi ya
watoto.
“Ukiwa mwanaharakati ukisema hiki sio kizuri
unaonekana huna adabu,” anasema Adelina.
Kutokana na kasumba hii wamekuwa wakinyimwa nafasi
ya kuzungumza kwenye majukwaa mbalimbali na wakati mwingine kwenye yale
machache wanayopatiwa nafasi wameishia kuzomewa kwamba wanapoteza muda.
Shule na uana harakati
Lakini swali linaloweza
kuibuka ni je, mabinti hawa wanawezaje kugawa muda wao katika masomo na
shughuli zao za kutetea haki za watoto?
Mama yao anasema kuwa,
kutokana na shughuli zao kugusa jamii, na maisha ya kila siku, hivyo wakiwa
shule, hasa wakati wa mapumziko, wao huendelea kutoa elimu kwa wenzao.
"Wanapofunga shule, ndio
wanakuwa majukwaani au kwenye vyombo vya habari na matamasha mbalimbali,"
anasema.
Ndoto yao
Hata hivyo, mbali na harakati zao, bado watoto hawa
wana ndoto ya kufika mbali zaidi katika masomo yao. Adela asema yeye ndoto yake
ni kuwa mwanasheria, huku Adelina nae, akitamani kuwa mhandisi wa ndege.
.jpeg)

