NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Mhe.Patrobas Katambi,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) leo Januari 15,2024 jijini Dodoma.
MWENYEKITI wa TALGWU Taifa Bw.Tumaini Nyamhokya,akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) leo Januari 15,2024 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Ndg. Rashid Mtima,akitoa taarifa ya Kikao cha Baraza Kuu TALGWU Taifa kilichofanyika leo Januari 15,2024 jijini Dodoma.
sehemu ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) leo Januari 15,2024 jijini Dodoma.
JOHN BANDA, DODOMA
Naibu Waziri Ofisini ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu , Mhe. Patrobas Katambi amewataka waajiri kuhakikisha wanafuata matakwa ya sheria za kazi za nchi na kudumisha mahusiano mema kazini kwa manufaa yao wenyewe na wafanyakazi wao.
Katambi ameyasema hayo Leo Januari 15,2023 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao Cha Baraza Kuu la chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) chenye lengo la kupitia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Chama hicho, taarifa ya fedha kwa mwaka 2023 pamoja na kufanya kazi ya kupitia na kuidhinisha makisio ya mapato na matumizi ya Chama hicho kwa mwaka wa fedha 2024.
Ambapo Katambi ,amesema Serikali itaendelea kulinda na kuendeleza haki za wafanyakazi nchini huku ikitambua, kuheshimu na kuuenzi mchango wa Watumishi wa Umma ambao ni Wanachama TALGWU.
"Waajiri kuhakikisha wanafuata matakwa ya sheria za kazi za nchi na kudumisha mahusiano mema kazini kwa manufaa yenu wenyewe na wafanyakazi wenu na Utashi wa Serikali katika kutekeleza wajibu wake wa kulinda haki za wafanyakazi nchini umejidhihirisha wazi kupitia hatua za kisheria na za kiuchumi ambazo imekuwa inatekeleza,"
Na kuongeza kuwa"Tunatambua kuwa wengi wenu mnafanya kazi katika mazingira magumu lakini Serikali haitachoka kuzifanyia kazi kero na changamoto zenu na kutafuta njia mbalimbali za kuzipatia ufumbuzi sambamba na kuendelea kuboresha mazingira ya kazi,"amesema Katambi
Awali Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Rashid Mtima,ameiomba serikali kutatua changamoto na kero zinazowakabili ikiwemo changamoto ya kulipa Leseni ya kutoa huduma kwa watumishi wa kada ya Afya.
Bw.Mtima amesema kuwa kuna manung’uniko na malalamiko makubwa kwa watumishi wa kada ya Afya yaani Wauguzi, Wafamasia, Wataalamu wa Maabara, Wataalamu wa Mionzi na Wafiziothelapia kutakiwa kujilipia ada ya Leseni ya kila Mwaka huku wa kuwa wanatekeleza majukumu ya kutoa huduma kwa umma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TALGWU Taifa Bw.Tumaini Nyamhokya amesema kuwa kuna kilio Kikubwa cha wafanyakazi walio na elimu ya darasa la Saba ambao mishahara yao kati ya miezi mitatu hadi sita haikulipwa ,zile siyo fedha za hisani ni mishahara yao lakini pia na hata walivyosimama walisimama kimakosa kwani hata barua zao tunazo.
“Iwapo watashindwa kulipa ada hiyo wanakosa haki ya kupandishwa madaraja na kushindwa kubadilishwa vyeo, ikumbukwe kuwa watumishi hawa hawafanyi biashara kwa leseni hizo isipokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kila siku kwa maendeleo ya Taifa letu” amesema Bw.Mtima
Akijibu Changamoto hizo Naibu Waziri Katambi amewahakikishia TALGWU kuwa Serikali imesikia, imeelewa na ipo tayari kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wafanyakazi wanatekeleza majukumu yao kwa amani huku changamoto walizonazo zikiwa zinapatiwa ufumbuzi na serikali chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia amewataka wanachama wote wa TALGWU kutambua kuwa ulinzi wa haki za wafanyakazi huanzia kwa wao wenyewe kwa kuzingatia dhana ya haki na wajibu,hivyo Chama hicho kinapaswa kuwakumbusha wafanyakazi kujiepusha na vitendo vinavyoenda kinyume na misingi na maadili ya Utumishi wa Umma.
"Wafanyakazi kama hawatajiepusha na matendo hayo maovu basi watafanya kazi ya kutetea na kulinda haki zao kuwa ngumu kwao na wadau wengine kama sisi. Lazima wakati wote tukumbuke kuwa kudai haki kunaenda sambamba na kutimiza wajibu,"amesisitiza Katambi







