BANDA MEDIA BLOG

Utengezaji vyungu na matumizi yake unavyopotea katika jamii

Fathiya Bayusuf

Mombasa, Kenya

Katika eneo la Jomvu Kuu, mjini Mombasa, pwani ya Kenya, nakutana na Time Mwinyi, mwenye umri wa makamo, akihusika na usafi wa nyumbani wakati wa asubuhi. Baada ya kumaliza majukumu yake ya kila siku, anaelekea kazini kwake, ambapo ni karibu na nyumbani kwake. Hapa, anajumuika na wanawake wenzake na kushiriki nao katika kazi ya kufinyanga vyombo vya udongo.

Sanaa ya kufinyanga vyungu na bidhaa za udongo ni ujuzi wa kiasili unaothaminiwa sana na watu wa eneo hilo, haswa wanawake wa Jomvu. Ustadi wao wa kufinyanga vyungu, vikaango, na vyetezo unachangia kwa kiasi kikubwa utamaduni wa Mswahili.

Kwa mujibu wa Bi. Mwinyi, ujuzi huu wa asili walioupokea kutoka kwa wazee wao umewawezesha kudumisha utamaduni wao na pia kujipatia kipato cha kujikimu maishani.

Tija kwa kina mama

"Ujuzi huu umetufikisha mbali, umetokana na mafundisho ya wazee wetu wa zamani, na sisi tunajitahidi kuendeleza na kufundisha vizazi vijavyo. Ni fursa nzuri sana kwa sababu, tunaweza kuviuza na kujipatia kipato kinachotusaidia katika kusomesha watoto wetu na kutoa mahitaji ya familia," anasema Bi. Time Mwinyi, ambae anasifika kwa uhodari wake katika ufinyanzi huko Jomvu Kuu.

Kina mama hawa wanashirikiana kwa pamoja katika shughuli zao za kila siku. Hatua ya kwanza ni kuchanganya udongo na mchanga maalum, na kisha kuongeza maji na kulaza kwa muda ili viweze kuchanganyika vizuri. Udongo unapokuwa tayari, wanaukanda kama unga wa ngano wa kupikia ili kupata muundo mzuri.

"Hatua inayofuata ni kuunda mnara maalumu kwa kuuinua udongo, na sehemu ya ndani huchukuliwa ili kupata umbo la chungu. Kipande cha shaza kilichochovya maji hutumika kulainisha sehemu ya ndani ya chungu. Kisha, kwa umakini mkubwa, chungu kilichokamilika hukatwa na kuwekwa juu ya jiwe. Shughuli hii inahitaji ustadi na umakini, vinginevyo chungu kinaweza kuharibika," anaeleza Time Mwinyi.

Jinsi ya kufinyanga vyungu

Vyungu hivyo vinawekwa pembeni ili vikauke, na mfumo huo pia hutumika kutengeneza vyombo vingine vya udongo kama vile chetezo, kiana, na kikaango.

"Baada ya kukausha, sehemu ya chini ya vyungu hukatwa na kuundwa umbo zuri. Tunaweka mapambo kidogo juu yake, na kisha tunaitengeneza vizuri kwa kutumia upawa. Vyungu hivi hupangwa na kusafishwa kwa umakini na hatimaye kuwekwa juani," anasema Time Mwinyi.

Baada ya kukauka juani, vyungu huchomwa kwenye makumbi ya mnazi na nyasi maalum kwenye eneo la jochoni. Hii ni kutokana na joto na moshi unaohitajika.

"Tunapoweka vyungu jochoni kwa masaa kadhaa na vinapokuwa tayari, tunavichukua nje na kuviweka pembeni mpaka vipoe. Baada ya hatua hiyo, bidhaa zinakuwa tayari kutumika au kuuzwa," anasema Bi. Time Mwinyi.

Baada ya kukamilisha mchakato wa kufinyanga, bidhaa hizo hupelekwa kwa wafanyabiashara katika soko la vyungu maarufu la Mwembe Tayari, Mombasa. Wengi wa wafanyabiashara hao ni wanawake, ingawa matumizi ya vyungu yamepungua kutokana na ushindani na vifaa vya kisasa kama masufuria ya chuma, vyetezo vya umeme, na vinginevyo.

"Biashara ya vyungu imepungua kidogo tangu kuingia kwa vifaa vya kisasa kama masufuria. Hivyo, tumelazimika kuongeza bidhaa nyengine kama miko, uteo, matuguu, majamvi, na kuendelea. Hata hivyo," anasema Kulthum Shenga Khamis, mfanyabiashara wa vyungu.

Umuhimu wa vyungu

Wajomvu bado wanasisitiza umuhimu wa vyungu na vyombo vya udongo dhidi ya vifaa vya kisasa. Wanaamini kuwa vyungu vinafaida nyingi katika mapishi na afya. Tofauti na sufuria za kawaida, vyungu huchemsha chakula taratibu, hivyo kukifanya kiwe kitamu zaidi. Vikaango hutumiwa kupikia mchuzi au mapishi mengine, na chetezo hutumika kufukizia nguo au nyumba.

"Huwezi kulinganisha chungu na sufuria, kwani chungu kinadumu na hakipozi chakula mapema kama ilivyo kwa sufuria. Vifaa vingine kama kikaango kinaweza kuongeza ladha ya kipekee kwenye mchuzi wako. Kiana kinaweza kutumika kama mfiniko, na bidhaa nyengine kama maziga kinaweza kutumika kama gesi la kupikia kwa kutumia kuni au makaa," anasisitiza Bi. Time Mwinyi.

Kutokana na changamoto za kupotea kwa ujuzi wa kiasili wa kufinyanga vyungu na bidhaa za udongo, wanawake hawa wameungana na kuunda chama chao. Chama hicho kina lengo la kuhifadhi utamaduni wao kwa kufundisha vizazi vijavyo na kushiriki katika matamasha ya kitamaduni yanayoandaliwa katika Kaunti ya Mombasa na maeneo mengine.

 







 

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG