BAADA Mzee wa Rukhsa kuwajibika Kwa kujiuzuru Uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere alimteua kuwa Balozi,
alipelekwa Balozi Nigeria kisha Misri ambako alikaa hadi Oktoba 1981 aliporejea nyumbani. Aliteuliwa Waziri wa Maliasili na Utalii na baadae Waziri wa Nchi ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano ambapo Ofisi zake zilikuwa Zanzibar.
Katika kuhamia Zanzibar anaelezea alivyofurumshwa na Jackson Makweta ambaye alipangiwa kukaa kwenye nyumba yake huko Oysterbay kiasi akamzuia asichukue vifaa vya ujenzi ambavyo alikuwa akitumia kujengea nyumba yake binafsi huko Mikocheni vilivyokuwepo hapo .
Hata hivyo anasema baadae alikuja kumteua kuwa Waziri baada ya kupata Urais. Hii inadhihirisha Mzee Rukhsa si mtu wa visasi.
Mzee Rukhsa anaelezea kuchafuka kwa hali ya siasa za Zanzibar Iliyopelekea Alhaj Aboud Jumbe avuliwe Urais wa Zanzibar mwaka 1984 na yeye kupendekezwa Rais wa mpito na baadae kugombea na kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar. Ameeleza namna alivyomteua Hayati Seif Shariff Hamad kuwa Waziri Kiongozi. Amemuelezea Seif kama mtu mwenye hulka ya kutaka madaraka na kwamba alimvumilia sana. Ameeleza namna alivyotawala Zanzibar na kuleta mabadiliko kwa muda mfupi na hasa kwenye kufungua milango ya upatikanaji wa bidhaa kiasi hata watu wa Bara walikuwa wanaenda Zanzibar kununua bidhaa. Pia aliongeza mishahara; anasema kuwa dhana ya Rukhsa ilianzia hapo.
Baada ya Mwalimu kuamua kuachia Urais anaelezea namna alivyopata nafasi ya kuteuliwa kugombea Urais wa Muungano, anaweka wazi kuwa hakuwa chaguo la Nyerere na kwamba Salim Ahmed Salim ndiye alikuwa chaguo lake. Salim aliponzwa na siasa za chuki za Wazanzibari wakimtuhumu kuwa ni Hizbu na kuwa alikula njama za kumuua Karume.
Katika kitabu ameeleza kiundani namna Siasa ya Ujamaa na Azimio la Arusha ilivyotekelezwa na hasa matatizo yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wake ikiwemo Operesheni Vijiji, Operesheni Maduka, Matatizo ya Mashirika ya Umma, Sheria ya nguvu kazi, Uhujumu Uchumi nk. Ameeleza namna Mageuzi ya Kiuchumi yalivyokuwa ya lazima.
Amejitahidi kuelezea hasa kipindi cha mwaka 1980 -1985 ambapo hali ya uchumi ilikuwa ngumu baada ya vita ya Uganda iliyoligharimu Taifa dola milioni 600. Kulikuwa na matatizo pia ya mashirika ya Umma ambapo mashirika mengi yalikuwa na matatizo ya uendeshaji uliotokana na uzembe, mengi yakiwa hayazalishi kutengeneza faida bali yakitegemea ruzuku kutoka Serikalini.
Pia ameeleza namna nchi ilivyokabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni kiasi alifikia nchi kuuza Mali kwa Mali ( barter trade).
Mzee Rukhsa anasema hali aliyoikuta ilikuwa ngumu kiasi kwamba hakuwa na namna nyingine bali kuchukua hatua kama alivyofanya, Anasema yeye si mtu wa nadharia bali vitendo.
Kitu cha kwanza alichofanya ni kuwataka Wafanyabiashara wenye mitaji kuleta bidhaa na kuwaahidi kuwa wasingeulizwa fedha wameipata wapi. Hali hiyo ilisababisha ahueni baada ya bidhaa kuanza kupatikana madukani. Baadae walibadilisha sheria ili kuondoa ukiritimba wa Benki Kuu kudhibiti fedha za kigeni na Kuanzisha maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.
Kuhusu mashirika ya Umma anasema mashirika mengi yalikuwa hayatengenezi faida, anatolea mfano wa UDA kuwa pamoja na kuwa na ukiritimba wa Usafirishaji katika jiji la Dar es salaam ilikuwa haiwezi kutoa huduma stahiki na ndipo wakaamua kuleta Chai Maharage ambapo magari madogo ya mizigo yalifanyiwa marekebisho kuweza kubeba abiria, anasema jina hilo lilitokana na mpangilio wa viti kama wa mabanda ya Mama Ntilie ambapo kifungua kimya maarufu enzi hizo kilikuwa chai maharage. Anasema baadae magari hayo yalipotea yenyewe sokoni kutokana na nguvu ya soko.
Katika kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni aliendeleza mazungumzo na IMF, mazungumzo ambayo yalikuwa yameanza wakati wa Nyerere lakini yakakwama kutokana na msimamo mkali wa Nyerere hasa kuhusu kushusha thamani ya sarafu yetu. Masharti mengine yalikuwa kufanya marekebisho katika riba za benki na kurekebisha mashirika ya Umma, kuchangia huduma za jamii kama Elimu na Afya. Anasema baada ya majadiliano IMF walitoa mkopo ambao ulileta ahueni kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu kupiga mnada Mashirika ya Umma anasema hatua iliyochukuliwa ilikuwa ni lazima kwa kuwa mashirika yalikuwa mzigo mzito kwa wananchi na kuwa yalikuwa yameajiri kuliko uwezo pia anasema baada ya kubinafsisha faida na tija ilipatikana anatolea mfano wa CRDB na TBL.
Baada ya Ahueni hiyo ya Kiuchumi kuanza kuonekana kama Mzee wa Rukhsa kueleza kwenye Kitabu cha Maisha Yake, Hapa BANDA MEDIA ONE.COM Tunaendelea kukuchambulia hatua kwa hatua, usikose Sehemu inayofuata....!!!
