#Takwimu zinaonyesha kwamba sekta hizi za mifugo na uvuvi ambazo kwa tafsiri za kimataifa za kitakwimu zipo ndani ya sekta pana ya kilimo inayotoa ajira kwa takriban asilimia 65 ya Watanzania.
#Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya SMT imekuwa na ushirikiano na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar na Wizara ya Kilimo, Maliasili Mifugo na Umwagiliaji. Ushirikiano huo umekuwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo, utayarishaji wa miradi ya pamoja ya maendeleo.
#Baadhi ya miradi hiyo ni; mradi wa MACEMP (2005-2012) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 61, mradi wa Swiofish (2010-2022) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 36 na mradi wa TASFAM (2023-2028) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 117.
#Katika hatua zote za utayarishaji wa Mradi wa Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi ambayo inatekelezwa katika pande zote mbili za muungano. Kwa sasa serikali inakamilisha mchakato wa ununuzi wa meli nane zitakazokuwa zinaendesha uvuvi wa kibiashara katika EEZ na Bahari Kuu.
#Meli hizo zitagawanywa kwa TAFICO (meli 4) na Shirika la Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) litapata meli 4 kupitia Programu ya AFDP inayofadhiliwa na IFAD.
#Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) ni Taasisi ya muungano. Wizara kupitia mamlaka hiyo imefanya maboresho katika kanuni za Sheria Uvuvi wa Bahari Kuu na kupandisha utoaji wa vibali vya uvuvi katika Bahari Kuu kutoka meli 9 mwaka 1988 hadi meli 61 mwaka 2023/24 kwa ajili ya kufanya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) upande wa Tanzania.
#Tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya DSFA hadi mwaka 2021/2022, jumla ya meli za uvuvi 502 zimepatiwa leseni zenye thamani ya shilingi bilioni 24.31 ambapo jumla ya tani za ujazo 67,437.90 za samaki zilivuliwa katika EEZ ya Tanzania kwa wastani wa tani 6,130.7 kwa mwaka.
#DSFA pia imeingia mkataba na Kampuni ya Albacora ya nchini Hispania kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki katika mkoa wa Tanga. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 20 za samaki kwa siku, kuhifadhi tani 2,400 za samaki na kuajiri wafanyakazi zaidi ya 100.
#Serikali ya Awamu ya Sita ilianzisha Program ya Jenga Kesho Iliyobora ambapo vijana na wanawake 200 wamewezeshwa kupata mafunzo ya ujasiriamali, mbinu bora za uvuvi na ukuzaji viumbe maji ambao wamehitimu kwenye awamu ya kwanza.
#Aidha, vijana na wanawake 300 wanaendelea na mafunzo katika awamu ya pili ambapo kati ya hao vijana 50 ni kutoka Zanzibar.
#TAFIRI inashirikiana na ZAFIRI kwenye maeneo mbalimbali, taasisi hizi mbili zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa muda mrefu wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya TAFIRI. Ushirikiano huu umejengwa kwenye msingi muhimu kwamba samaki hawajui mipaka, hivyo pamoja na kuwa uvuvi siyo jambo la muungano, bado ushirikiano kwenye utafiti na usimamizi wake ni muhimu.
#Wizara ya Mifugo na Uvuvi inashirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kuendesha kiwanda cha kuchakata mwani kilichopo Zanzibar chenye uwezo wa kuchakata tani 30,000 kwa mwaka kwa kuongeza upatikanaji wa malighafi ya mwani kutoka Tanzania Bara ambapo kwa sasa uzalishaji wa zao hili kwa Tanzania Bara umefikia tani 8,343.75.
#Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukitumia Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Machui Tanga kupata vifaranga vya samaki na viumbe maji wengine wakiwemo jongoo bahari kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa buluu.
#Kutokana na uwepo wa kiwanda hicho, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya TADB, imewakopesha wakulima wa mwani mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba kwa kuwapatia vifaa na pembejeo za kilimo cha mwani ambapo jumla ya shilingi 447,000,000 zilitumika kwa kukopesha kamba za mwani 22,983, tai tai 102,911 na mbegu za mwani kilo 228,805, mambo/vigingi 137,215 na viroba/mifuko 1,029.
#Sekta ya uvuvi inakua kwa asilimia 1.9 na imechangia asilimia 1.8 katika Pato la Taifa kwa mwaka 2022, ni miongoni mwa sekta tatu za kilimo ambazo zinaajiri wananchi wengi na imeweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji wapatao 35,986.
#Aidha, zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanakadiriwa kupata kipato chao cha kila siku kutokana na shughuli za uvuvi huku idadi ya wavuvi wadogo ikiongezeka kutoka wavuvi 75,621 mwaka 1995 waliokuwa wanatumia vyombo vya uvuvi 22,976 hadi wavuvi 198,475 waliotumia vyombo 58,820 mwaka 2023.
#Aidha, kiasi cha samaki kilichozalishwa kiliongezeka kutoka tani 255,900.74 za samaki zenye thamani ya shilingi 70,467,575.96 mwaka 1995 hadi tani 479,976.6 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 mwaka 2023.
#Serikali imewezesha utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi - Kilwa Masoko wenye thamani ya shilingi bilioni 289.5 na tayari kiasi cha shilingi bilioni 106.23 kimetolewa. Ujenzi umefikia asilimia 52 na ajira za moja kwa moja 278 zimetolewa kwa wananchi katika eneo la mradi.
#Kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa-Masoko kutawezesha: Meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania (EEZ) na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa; kuchochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi; kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi; na kuchangia katika pato la Taifa.
#Sekta ya mifugo ni miongoni wa sekta za kiuchumi na uzalishaji ambayo inatoa ajira kwa wananchi wengi wa Tanzania, ilikua kwa asilimia 5.0 na mchango wa sekta katika pato la Taifa (GDP) ulifikia asilimia 6.7 kwa mwaka 2022.
#Uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 97,000 mwaka 1964 hadi tani 738,166 mwaka 2023, hii imetokana na kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama kutoka kiwanda kimoja mwaka 1964 (Tanganyika Parkers) kilichokuwa na uwezo wa kuchinja ngombe 800 kwa siku hadi viwanda 11 vyenye uwezo wa kusindika tani 337 kwa siku.
#Kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya hivi karibuni, mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/21 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2022/23 na kufanya jumla ya tani 35,297 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 146.43 zilizouzwa nje ya nchi.
#Uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 334,000 mwaka 1964 hadi lita bilioni 3.4 mwaka 2022/2023 na usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka wastani wa lita 41,026,000 kwa mwaka 1964 hadi wastani wa lita milioni 75.9 kwa mwaka 2023. Aidha, viwanda vya kusindika maziwa pia vimeongezeka kutoka viwanda saba vya umma mwaka 1974 hadi kufikia viwanda vya sekta binafsi 105 mwaka 2023.
#Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliweza kutokomeza mbung'o na ugonjwa wa Nagana katika kisiwa cha Unguja kwa kutumia mbung'o hasi ambao walizalishwa katika maabara ya Kituo cha Utafiti wa Mbungo na Ndorobo kilichopo Tanga.
#Serikali ya Awamu ya Sita imetoa kiasi cha shilingi bilioni 51.66 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali katika sekta ya mifugo ikiwemo, ujenzi wa miundombinu ya minada ya mifugo ya kisasa 51 shilingi bilioni 17.5, ujenzi wa majosho 746 kwa gharama ya shilingi bilioni 15.92 katika Halmashauri mbalimbali nchini na ujenzi wa vituo 10 vya kukusanyia maziwa kwa shilingi bilioni 2.5.
#Ujenzi wa mabwawa 15 kwa shilingi bilioni 8.04 kwenye Halmashauri mbalimbali nchini, ujenzi wa miundombinu katika vyuo vya mafunzo ya mifugo shilingi bilioni 4.4 ambao umehusisha ujenzi wa Hosteli mbili (2) zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 424 kila moja na kumbi 10 za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 hadi 150 kila mmoja na ujenzi wa miundombinu ya maabara ya uzalishaji wa chanjo za mifugo wenye thamani ya shilingi bilioni 5.6.
#Udumu muungano wetu na yadumu maono ya waasisi wetu kwa kuwa muungano wetu ni tunu yetu na sisi lazima tujifaharishe na yaliyoasisiwa na viongozi wetu. Yeyote anatakayeonekana yuko kinyume na muungano wetu, ni adui yetu.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*



