.........................................................................
NA JOHN BANDA, DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema
hadi kufikia Juni mwaka jana serikali ilikuwa imetoa sh. bilioni 696.7 kwa
ajili ya kupunguza na kuondoa umaskini kwa kaya zipatazo milioni 1.37
katika vijiji, mitaa na shehia 17,260.
Simbachawene amesema
hayo jijini hapa jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
mafanikio ya wizara hiyo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema lengo la
Serikali ya Awamu ya Sita na awamu zilizopita zinazoongozwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ni kupunguza na kuondoa umaskini wa kipato.
Amesema Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na serikali mwaka 2000 kama
mojawapo ya mikakati ya kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya
ushirikishaji jamii.
“TASAF imekuwa
ikitekelezwa kwa awamu tangu kuanzishwa kwake. Awamu ya Kwanza ya
TASAF ilianza mwaka 2000 – 2005 na ilijumuisha maeneo ya utekelezaji 42
ambapo 40 ni ya Tanzania Bara na mawili ya Zanzibar (Unguja na
Pemba).
Ameongeza kuwa :”Jumla
ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya sh. bilioni 72 ilitekelezwa
kupitia mpango huu wa TASAF I. Awamu hii ilitekelezwa kwa mafanikio
makubwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii katika sekta
mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, miundombinu na afya,”.
Simbachawene
alisema awamu ya Pili ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005
hadi 2013 katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania
Zanzibar.
Amefafanua kuwa
jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430
ilitekelezwa wakati wa Awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).
“Katika kipindi cha utekelezaji wa TASAF Awamu ya Kwanza na ya Pili, wananchi walishiriki vyema kutekeleza miradi mbali mbali iliyoboresha upatikanaji wa huduma za jamii. Mbali na miradi ya kuboresha miundombinu kama vile barabara, maji, masoko, huduma za afya, elimu, ustawi wa jamii na mazingira, wananchi katika makundi mbali mbali walitekeleza miradi ya kuongeza kipato ambayo iliwasaidia kukabiliana na umaskini.
Ameongeza kuwa :”Katika
Kipindi cha Pili hadi kufikia Juni 2023 kiasi cha sh. bilioni 696.7
zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,371,916 katika vijiji, mitaa na
shehia 17,260,”
TAKUKURU
Simbachawene amesema katika
miaka 60 ya Muungano, serikali inayoongozwa na Rais, Dk. Samia Suluhu
Hassan inaendelea kutekeleza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa ili
wananchi waweze kupata huduma bora.
Alisema TAKUKURU
kwa kutambua kuwa Skauti ni suala la Muungano kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya
kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST), ZAECA na TAKUKURU
ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa.
“Ushirikiano huu ni
muhimu sana kwa ustawi wa Taifa kwa kuwa Skauti wapo katika kundi la vijana na
ni “Jeshi kubwa” ambalo tumeshuhudia likitoa mchango chanya katika matukio
mbalimbali ya kijamii na kitaifa,”alisema .