Na Mwandishi
wetu,
Wapiga kura 11,936 wanatarajiwa kupiga kura kesho tarehe 09 Juni, 2024 kwenye
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi, Zanzibar.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs
Mwambegele ameyasema hayo leo tarehe 07 Juni, 2024 jijini Dar es Salaam wakati
akisoma risala kwa ajili ya uchaguzi huo na kuongeza kwamba uchaguzi utahusisha
vituo 29 vya kupigia kura.
“Jumla ya wapiga kura 11,936 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) watashiriki katika uchaguzi huu
mdogo na jumla ya vituo 29 vya kupigia kura vitatumika,” amesema Jaji
Mwambegele.
Wagombea wanaowania Kiti cha Ubunge jimbo la Kwahani majina yao na vyama katika
Mabano ni Bw. Bashir Yatabu Said (Demokrasia Makaini), Bi. Nuru
Abdulla Shamte (DP), Bi. Mwanakombo Hamad Hassan (NLD), Bi. Zainab Maulid
Abdallah (CCK), Bi. Tatu Omary Mungi (UPDP), Bw. Khamis Yussuuf Mussa (CCM) na
Bi. Jarade Ased Khamis (AAFP).
Wengine ni Bw. Kombo Ali Juma (NRA), Bi. Shara Amran Khamis (ADC),
Bi. Naima Salum Hamad (UDP), Bi. Madina Mwalim Hamad (ADA TADEA), Bw. Amour
Haji Ali (SAU), Bi. Mashavu Alawi Haji (UMD) na Bw. Abdi Khamis Ramadhan (CUF).
Mwenyekiti wa Tume amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala wa vyama,
wapiga kura na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba hawapigi kampeni siku ya
kupiga kura kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
“Alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi,
bendera na mavazi haviruhusiwi kutumika kesho tarehe 08 Juni, 2024 ambayo ni
siku ya uchaguzi,” amesema.
Jaji Mwambegele ameongeza kwamba zoezi la kupiga kura katika maeneo yote ya
uchaguzi litafanyika katika vituo vilevile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi
Mkuu wa Mwaka 2020.
Ameongeza kwamba vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja kamili (1:00)
asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.
“Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao
wamefika kabla ya saa kumi kamili (10:00) jioni katika mstari na hawajapiga
kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari
wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni,” amesema.
Jaji Mwambengele amebainisha kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu
ambao walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Amesema, Tume imeandaa majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura
kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kupiga kura bila usaidizi.
Aidha, Kwa wapiga Kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada
hayo, wataruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya
kuwasaidia kupiga kura.
“Katika kituo cha kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu
wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokwenda na
watoto kituoni,” amesema.
Kuhusu wapiga kura kurudi nyumbani baada ya kupiga kura, Jaji Mwambegele
amesema hilo ni sharti la kisheria na kwamba maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa
na kuridhiwa na vyama vyote vya siasa, Serikali na Tume yanaelekeza hivyo.
Alisisitiza kwa kusema “wapiga kura watatakiwa kuondoka kituoni mara
wanapomaliza kupiga kura ili kuepusha msongamano na vitendo vinavyoweza
kuchochea uvunjifu wa amani. Hivyo, Tume inawashauri wananchi
kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura”.
Ametoa rai kwa wapiga kura katika Jimbo la Kwahani, kujitokeza kwa wingi kwenye
vituo vya kupigia kura, ili kuwachagua viongozi wanaowataka.