Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaaguzi Tanzania. Picha/INEC
Vyama vya siasa nchini Tanzania vitaruhusiwa kuweka
wakala mmoja kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura kwenye zoezi la
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaotarajiwa kuzinduliwa mkoani
Kigoma, tarehe 01 Julai, 2024.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi (INEC), Jaji (Rufaa), Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa
Tume na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam Juni 7,
2024 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari.
“Leo kila chama kitapewa nakala ya orodha ya vituo
vyote vya kuandikisha wapiga kura. Dhumuni la kuwapatia nakala hizo ni
kuwawezesha kupanga na kuweka mawakala wa uandikishaji katika vituo vya
kuandikisha wapiga kura,” amesema na kuongeza.
“Kila chama kitaruhusiwa kuweka wakala mmoja kwenye
kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa zoezi
la uboreshaji kituoni ikiwemo kuwatambua wale wanaokuja kituoni kama wana sifa
za kuandikishwa.”
Jaji Mwambegele amesema kwamba kikao hicho ni sehemu
ya utamaduni wa Tume iliojiwekea wa kuwashirikisha wadau wa uchaguzi wakati wa
utekelezaji wa majukumu yake.
Aliwataja wadau hao kuwa ni pamoja na viongozi wa
vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakilishi wa asasi za kiraia, wahariri wa
vyombo vya habari, waandishi wa habari, maafisa habari wa mikoa na halmashauri,
wawakilishi wa makundi mbalimbali ya vijana, watu wenye ulemavu na wanawake.
”Niwaombe viongozi wa vyama vya siasa kwa umoja wenu
kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya Tume kuhusu
zoezi la uboreshaji wa Daftari. Tume kwa upande wetu tutazingatia Katiba,
sheria ya uchaguzi na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi hili la
uboreshaji,” amesema.
Kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima, R. K amesema kuwa pamoja na kufanyika kwa
uzinduzi tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa
kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, uboreshaji wa Daftari utaanza siku hiyo mkoani
Kigoma na kuendelea kwa siku saba hadi tarehe Julai 7, 2024.
”Kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi,
uboreshaji utafanyika kwenye mizunguko 13 itakayobainishwa kwenye ratiba.
Aidha, zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha
wapiga kura,” amesema.
