
Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimekabidhi kambi ya jeshi ya Abdalla Birolle kwa Wanajeshi wa Kitaifa wa Somalia (SNAF).
Kambi hiyo ya kijeshi, ambayo hapo awali ilikuwa chini ya Wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya wa ATMIS (KDF), ni ya nne kukabidhiwa kama sehemu ya mchakato uliopangwa.
Naibu Mwakilishi Maalum ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (DSRCC), Siyuvile Bam, aliongoza tukio la kukabidhiwa kwa kambi hiyo ya kijeshi.
Katika tukio hilo, miongoni mwa walikuwapo ni wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN) na maafisa wa Jimbo la Jubaland.
"Somalia iliwahi kutoa hifadhi kwa wapigania uhuru kutoka nchi nyingine za Afrika wakati wa harakati zao za kutafuta uhuru. Ni wajibu wetu kurudisha uungwaji mkono na kujitolea kwa watu wa Somalia kwa ajili ya uhuru wa nchi zetu," alisema Bw. Bam.
Aliongeza kuwa, "Ingawa tunakabidhi majukumu ya usalama, Umoja wa Afrika hautaitelekeza Somalia na utaendelea kuunga mkono mchakato wa amani na usalama unaoongozwa na Somalia."
"Kiutendaji, tumepata mafanikio makubwa, na kuwa na athari kubwa kwa usalama huko Kismayo. Kambi ya jeshi ya Abdalla Birolle inatumika kama eneo lisilo na vita uwanja wa ndege wa Kismayo na hivyo kwa wenzetu wanaochukua nafasi hii, tunawatakia kila la kheri. Tutaendelea kuwepo kwa mashauriano na msaada kama inavyohitajika," Brig Rashid alisema.
Akiwakilisha kikosi cha wanajeshi wa kitaifa wa Somalia, Meja Muhudin, alishukuru kikosi cha ATMIS, KDF kwa kujitolea kwao kuhakikisha usalama wa Somalia.
"Wanajeshi wa Jeshi la Kenya wamejitolea wakati muhimu kupigania ukombozi na usalama wa Somalia, na kuchangia katika mchakato wa amani. Hakuna anayehatarisha maisha yake isipokuwa kwa sababu muhimu," alisema Meja Muhudin.