Adeladius Makwega-MWANZA
Wakristo wameambiwa kuwa masomo ya dominika ya leo
yanasisitiza kila mwanadamu kumthamini mwanadamu mwenzake na ndiyo maana visa
viwili vinavyoonekana katika Injili ya leo vinaonesha Yesu alivyo msaada kwa
jamii mbili.
“Kwa Jina la Baba na La Mwana na la Roho
Mtakatifu-AMINA. Bwana Awe Nanyi- Awe Rohoni Mwako. Ndugu zangu karibuni katika
Adhimisho la Ekaristi Takatifu ndani ya dominika ya 13 ya Mwaka B wa Liturujia
ya Kanisa, wakati tunatafakari masomo ya misa hii kila mmoja atilie maana
namna Yesu Kristo alivyomfufua mtoto wa Jairo na namna alivyomponya mama
aliyekuwa akitokwa damu miaka kumi na miwili, mama huyu alipokea uponyaji
kutokana na imani yake nasi tukumbuke tutapokea uponyaji wetu kadili ya imani
yetu, kubwa sisi sote tumfanye Yesu Kristo kuwa kila kitu katika maisha yetu.”
Haya yamesemwa na Padri Samson Masanja Paroko wa
Parokia ya Malya-Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza katika misa ya kwanza iliyoanza
saa 12.07 ya asubuhi katika Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Wamisionari.
Padri Masanja alianua jamvi la mahubiri yake akisema
kuwa injili inaonesha Yesu Kristo anakimbilia na watu wote na kwake changamoto
zote zinatatuliwa, je wewe na mimi tunamkimbilia nani? Sote tukumbuke kimbilio
letu ni Yesu Kristo.
Katika misa hiyo hiyo ya kwanza ya jumapili umeme
ulikatika saa 7. 11 ya asubuhi na baadaye kurejea saa 7.13 wakati huo misa hii
ilikuwa katika kipindi cha MAGEUZO Padri Masanja aliweza kuendelea na MAGEUZO
vizuri maana mwanga wa jua ulisaidia yeye kuweza kuongoza misa hii japokuwa
ulikuwa mwanga hafifu.
Kwa sasa katika eneo la Malya na viunga vyake
kumekuwa na desturi ya umeme kukatikakatika na kurudi hata mara nne kwa siku
moja ambapo zoezi hilo ni hatari kwa vifaa va umeme, makazi ya watu na hata
watoto wanaozaliwa NJITI na kuhifadhiwa katika Ikubeta ndani ya Hospitali zetu.
