NA JOHN BANDA, DODOMA
IMEELEZWA kuwa Kila mwananchi ana jukumu la kumlinda mtu mwenye ulemavu au yule mwenye Mahitaji maalumu bila kujali tofauti kwani watu wote kwenye jamii ni sawa.
Hayo yamebainishwa June 29, 2024 na Kiongozi
wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava wakati alipotembelea na kugawa zawadi kwa
watu wenye mahitaji maalumu katika kituo cha kulelea watoto kilichopo kwenye
shule ya Msingi Bwigiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Kiongozi huyo amezungumza na baadhi ya wananchi
waliojitokeza katika eneo hilo na kusema kila mwananchi ana wajibu wa kumlinda
mwenzake hivyo haipaswi kuwanyanyapaa wala kuwatenga watu wenye mahitaji
Maalum kwani nao wana haki ya kuishi kama ilivyo wengine.
"Kuna baadhi ya watu bado wana imani potofu juu
ya watu wenye Ulemavu. Hata Serikali inatambua umuhimu wao kwani wana haki na
wajibu kama watu wengine. Tunatakiwa kuhakikisha tunaendelea kuitunza amani ya
watu hao"
"Tuendelee kuwalinda kwani wapo maharamia ndani
ya nchi hii ambao wanafanya ukatili na utakapoona viashiria hivyo, toa
taarifa mapema kwenye vituo vya Polisi vilivyopo karibu yenu" Amesema
Mzava.
Haki ya kupata upendo na Amani katika nchi hii ni ya kila mtu bila kujali kabila wala Dini.
Mwenge wa uhuru umekimbizwa katika wilaya ya Chamwino huku mradi mbalimbali ya maendeleo ikizinduliwa juni 29, ambapo juni 30 umepokelewa katika Halmashari ya Wilaya ya Kondoa.










