Askofu wa Dayosisi ya Rifty Valley mkoani Singida, John Lupaa akikabidhi msaada wa Godoro, Branket na Mahindi kilo 60, kwa mmoja wa wahanga wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizoambatana na upepo mkali, yaliyotokea mwezi januari mwaka huu katika kijiji cha sasajila wilayani Manyoni.
Katibu wa Ushirika wa Mama wa Kikristo (UMAKI) anayeshughulika na kuratibu Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Jamii. Lay Canon Dkt. Margareth Ndonde, akitoa msaada huo kwa mmoja wa waathilika
(PICHA ZOTE NA JOHN BANDA)
Baadhi ya wahanga wa Mafuriko yaliyosababishwa na Mvua za Upepo, wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kanisa Anglikana Tanzania, baada ya Kupokea Msaada wa Godoro, Mahindi kilo 60 kwa kila mmoja na Branketi la kujifunika.
(PICHA ZOTE NA JOHN BANDA)
............
NA JOHN BANDA, SINGIDA
KANISA Anglikana Tanzania, limetoa msaada wa Vyakula, Magodoro na Mabranketi yenye thamani ya Zaidi ya milioni 18, za Kitanzania kwa kaya Zaidi ya 120 zilizokumbwa na Kadhia ya mafuriko Januari kwaka huu katika Kijiji cha Sasajila kata ya chikuyu wilaya ya Manyoni Mkoani Singida.
Akiongea Julai 21,2024 nje ya Kanisa la Mtakatifu Methew, Anglikana Sasajila, mara baada ya kukabidhi Misaada hiyo Askofu wa Dayosisi ya Rifty Valley mkoani Singida, John Lupaa amesema kanisa Anglikana Tanzania kwa Kushirikiana na Dayosisi hiyo, wametoa msaada huo kwa wahanga waliokumbwa na mvua zilizoambatana na Upepo mkali.
Amesema Mvua hizo zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali za wakazi Zaidi 165, wanaotoka kaya 120 katika Kijiji cha Sasajila, kata ya Chikuyu wilayani humo ambapo Nyumba za makazi, Vyakula na mali nyingine viliharibiwa na kuwafanya wakazi hao kukosa makazi.
“kigezo kilichotumika kuwapa misaada hii ni kutokana na watu hawa kukosa makazi na vyakula kutokana na nyumba, mazao waliyokuwa wamelima kusombwa na maji wakati wa mvua hizo za mwezi januari mwaka huu”, amesema
Kwa Upande wake Katibu wa Ushirika wa Mama wa Kikristo (UMAKI) anayeshughulika na kuratibu Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Jamii. Lay Canon Dkt. Margareth Ndonde aliyemwakilisha Katibu Mkuu, wa Kanisa hilo, Canon Bethuel Mlula amesema moja ya kazi za kanisa ni kuwafikia watu wenye uhitaji, wakiwemo waliokumbwa na Madhila mbalimbali yakiwemo hayo yaliyosababishwa na mvua zilizoambatana na Upepo mkali.
“kanisa limetoa msaada wa vitu vyenye thamani ya sh. Milioni 18, tukijua msaada huo utawasogeza sehemu, maana wao hawakujitakia bali ni kutokana na majanga ya asili na kwamba tutaendelea kuwaombea”, amesema
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Weza B. Bonface Mahajile amesema msaada huo utatumika vizuri, kwa kuwa atahakikisha anawafuatilia wahanga 48, wanaotoka katika kitongoji chake ili kuhakikisha hakuna anayeuza au kutumia vibaya msaada huo uliotolewa na Kanisa la Anglikana Tanzania.
Nae Chapa Muganda mwenye asili ya kisukuma, akiongea kwa Kiswahili cha kubahatisha kutokana na kutokijua sawasawa na Anjelina Msangu wamelishukuru Kanisa la Anglikana kwa kuwapa msaada huo na kwamba chakula hicho kitawasogeza kwa Zaidi ya miezi miwili.
Mvua zilizoambatana na upepo zilisababisha mafuriko katika Mikoa ya Tanzania Kuanzia Januari mwaka huu, Mpaka katikati ya Mwezi wa Nne ambapo yalisababisha maafa makubwa, yakiwemo ya watu kupoteza Maisha, Mali, vyakula na nyumba za makazi na majengo ya Umma.