
Baraza Kuu la Waislamu nchini Tanzania (BAKWATA) kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake, Sheikh Mohamed Khamis, wameitaka serikali kupunguza gharama za matibabu pamoja na kuboresha maslahi ya walimu ili kuendelea kukuza nguvu za kiuchumi na kujenga jamii iliyoelimika kuelekea mwaka 2050.
Sheikh Khamis ametoa kauli hiyo Jumatatu, Januari 13, 2025, katika Mkutano wa Kamati ya Dini Mbalimbali Kuhakiki Rasimu ya Dira hiyo, uliofanyika Ukumbi wa TEC, Kurasini, Dar es Salaam, ikiwa ni Kundi la Mwisho kufikiwa na Tume ya Mipango kwaajili ya Mapitio ya rasimu hiyo.
Sheikh Khamis, amehimiza pia umuhimu wa serikali kusimamia ratiba na mapumziko kwa wanafunzi wa shule za Serikali na za binafsi kama sehemu ya kuhakikisha kuwa kunakuwa na ulinganifu wa masomo na mapumziko kwa wanafunzi.
Pia Bakwata wameiomba serikali kutenga viti vya uwakilishi wa Taasisi za kidini kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ulivyo uwakilishi mwingine kwenye chombo hicho muhimu cha kutunga sheria.
Aidha Bakwata wamehimiza umuhimu wa kutunza mazingira kuelekea mwaka 2050, kutungwa kwa mkakati wa kudhibiti bidhaa bandia pamoja na kuhamisha utalii wa ndani kwa kupunguza gharama za kutembelea vivutio vya utalii sambamba na kutoa ruzuku kwa taasisi zote zinazotoa huduma kwa jamii bila ya ubaguzi.