Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum Pardo, amekosoa matamshi yaliyotolewa na rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kuhusu kubadili jina la Ghuba ya Mexico kuwa "Ghuba ya Marekani", akipendekeza jina la Marekani libadilishwe na kuwa "Marekani ya Mexico".
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano, Rais wa Mexico alionyesha ramani ya dunia ya karne ya 17 inayoonyesha Amerika Kaskazini kama "Amerika ya Mexico" na kusema: "Sasa kwa kuwa Trump amezungumza juu ya jina ngoja na sisi pia tuzungumzie jina."
Sheinbaum Pardo ameendelea kwa kuuliza swali, kwa nini hatuiiti Marekani ya Mexoco na kusisitiza: "Ghuba ya Mexico ni jina linalotambuliwa kimataifa na katika Umoja wa Mataifa."
Awali, Waziri wa Uchumi wa Mexico pia alijibu matamshi ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump kuhusu kubadili jina la Ghuba ya Mexico kuwa "Ghuba ya Marekani" na kwamba nchi hiyo ya Amerika ya Kusini "inaendeshwa na magenge," akisema: "Jina la Ghuba ya Mexico halitabadilika; Je, ungependa kusaidia? Usitume silaha."
Waziri wa Uchumi wa Mexico, Marcelo Ebrard alisema katika mkutano na waandishi wa habari: "(Kauli za Trump) ni kama mimi nikisema, 'unamaanisha (magenge) yanatawala jimbo la Pennsylvania?' Maneno haya hayatatufikisha popote."
