Baba Mtakatifu Fransicko alizaliwa Disemba 17, 1936
mjini Buenos Aires. Yeye ni mtoto wa Mzee Mario na Mama Regina Sivori,
waliobahatika kupata watoto watano.
Katika ujana wake, alisoma na kufuzu na kuwa mtaalam
wa kemia, baadaye akaacha kazi hii na kujiunga Seminarini huko Villa Devoto.
Machi 11, 1958 alijiunga na malezi ya Kinovisi katika
Shirika la Majesuiti, akaendelea pia na masomo ya elimu dunia nchini Chile.
Disemba 13, 1969 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.
Kati ya mwaka 1970 hadi mwaka 1971 alikamilisha hatua
ya tatu ya majiundo yake kama Mjesuiti huko Hispania na Aprili 22, 1973 akaweka
Nadhiri za Daima.
Kati ya mwaka 1972 hadi mwaka 1973 alikuwa ni mlezi
wa Wanovisi, Jaalim, Mshauri na Gombera wa Chuo cha Massimo, Julai 31, 1973
akateuliwa kuwa Mkuu wa Jimbo la Argentina kwa upande wa Shirika, utume ambao
aliutekeleza kwa muda wa miaka 6.
Mwaka 1980 hadi mwaka 1986, alikuwa ni Gombera wa
Chuo cha Massimo na Paroko wa Parokia ya Patriaki San Josè, Jimboni San Miguel.
Mei 20, 1992 Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa
Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Buenos Aires, akawekwa wakfu kuwa Askofu Juni
27, 1992 na Juni 3, 1997 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo Kuu la
Buenos Aires na Februari 28,1998 akasimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la
Buenos Aires kufuatia kifo cha Kardinali Antonio Quarracino.
Februari 21, 2001 aliteuliwa kuwa Kardinali na Machi
13, 2013 alichaguliwa kuwa Baba Mtakatifu na alichagua jina la Papa Francisko,
ili kuendelea kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi katika huduma ya:
Amani, Maskini na mazingira.
HALI YA KIAFYA
Baba Mtakatifu Francisko alilazwa katika Hospitali ya
Gemelli iliyopo Roma.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa
anasumbuliwa na magonjwa mbalimbali, ambapo afya yake ilikuwa ikibadilika mara
kwa mara na alilazwa hospitalini hapo tangu Ijumaa Februari 14, 2025 hadi
alipotoka Machi 23, 2025.