Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya Shilingi 340,538,614,000 ambapo kati ya fedha hizo shilingi 294,998,588,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 45,540,026,000 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
Maombi ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara yaliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ambapo Bunge limepitisha na kuipongeza Wizara kwa jinsi ilivvyotekeleza majukumu yake kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na ilivyojipanga kutekeleza majukumu yake ikiwemo Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mhe. Balozi Kombo aliwaeleza Wabunge kuwa Wizara, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 imefanikisha kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kusimamia na kutetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi pamoja na kukamilisha mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 iliyozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 19 Mei 2025.
Mhe. Waziri Kombo amesema kuwa, Sera hiyo pamoja na mambo mengine inaweka msisitizo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ikiwemo kukuza upatikanaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, kutangaza na kuvutia fursa za uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, kuhamasisha ushiriki wa Diaspora katika maendeleo ya Taifa na kutumia Kiswahili kama nyenzo ya diplomasia kwa manufaa ya kiuchumi.
Pia amesema Sera hiyo imeweka msingi mpya wa kulinda mila, desturi na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo pia alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujumuisha malengo ya Sera ya Mambo ya Nje, Toleo la Mwaka 2024 katika mipango na programu zao.
