BANDA MEDIA BLOG

BI. AMINA AMUOMBA RAIS Dkt. SAMIA AMNUSURU NA TISHIO LA KIFO, ARUDISHIWE MASHAMBA YAKE

 

Bi. Amina Msigwa akionyesha baadhi ya miti iliyosalia, baada moja ya nyumba yake kubomolewa mwishoni mwa mwaka jana na watu wanaodaiwa kupanga njama za kumnyang'anya shamba lake lenye ukubwa wa heka 10
Bi. Amina Mohamed Msingwa akiwa na baadhi ya waukuu wake katika shamba lake linalodaiwa kupokwa na watu watatu.

                                               .......................................

       NA MWANDISHI WETU, HANDENI

AMINA Mohamed Msingwa mkazi wa Kijiji na kata ya Kang’ata wilaya ya Handeni Mkoani Tanga amemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kumsaidia kupata maeneo yake ya ardhi ambayo amenyang’anywa huku akiendelea kupewa vitisho vya kuuawa na wahusika na anapojaribu kuomba msaada ofisi za Kijiji Pamoja na kata anafukuzwa.

Akiongea na waandishi wa Habari waliofika kijijini hapo kujionea mazingira na hali halisi iliyopo, Bi. Amina amesema kuwa shamba moja lenye ukubwa wa zaidi ya Heka 10 alipewa na shangazi yake tena kwa maandishi mnamo mwaka 2009, katika ofisi ya mtendaji wa Kijiji.


Kwa Mujibu wa uthibitisho wa maandishi toka ofisi ya Mtendaji wa Kijiji hicho wa Tarehe 20. 11.2009 uliosainiwa na kugongwa muhuri wa Veo, ambao Bi. Amina aliwaonyesha waandishi wa Habari unaonyesha, Amina Mohamed Msingwa alikabidhiwa shamba lenye ukubwa wa heka 10 na shangazi yake Mwajuma Msingwa.

 Bi. Amina Msigwa akionyesha baadhi ya miti iliyosalia, baada moja ya nyumba yake kubomolewa mwishoni mwa mwaka jana na watu wanaodaiwa kupanga njama za kumnyang'anya shamba lake lenye ukubwa wa heka 10

Bi. Amina anasema mwaka 2012 serikali ya kata na Kijiji hicho ilimuomba kuwakatia wakazi watano waliokosa, makazi viwanja ili wajenge nyumba za kuishi katika sehemu ya shamba lake, kitendo ambacho hakukipinga akakubali wakapimiwa.

Pia Bi. Amina akaonyesha hati nyingine ya Mauziano ya shamba lenye ukubwa wa heka 8 ambalo alilinunua kwa ndugu yake Shabani Mohamedi Msingwa tarehe 17.01.2017 ambalo nalo alijitokeza mtu mwaka jana akitokea jijini Dsm, akaingia shambani humo akaanza kupiga sumu kwenye migomba na kisha kuchoma moto mbaazi alizokuwa amelima.

Bi. Amina Msigwa akionyesha migomba inayodaiwa kupuliziwa sumu, pamoja na baadhi ya mashina ya mbaazi yaliyochomwa moto, na watu wanaodaiwa kupanga njama za kumnyang'anya shamba lake lenye ukubwa wa heka 8 pamoja na la heka 10.

“niwaambie wanangu nilifika shambani siku hiyo nikaona kitendo hicho, nikakimbia kwa mtendaji nikawambia tukaongozana wakamkamata na kumpeleka kituo cha polisi Handeni ambapo hata kabla ya kufika akasema tunajisumbua hawawezi kukaa ndani kwa sababu serikali yote ya wilaya ipo mikononi mwake,

‘’Na kweli tulipofika kituo cha polisi Handeni, mkuu wa kituo akatufukuza akisema hiyo siyo kesi ya kupelekwa polisi hivyo turudi tukayamalize nyumbani”, anasema Bi. Amina.

Aidha Bi. Amina anasema kutokana na matukio hayo yakiwemo ya kupigwa mpaka kupoteza fahamu mwishoni mwa mwaka jana, kutishiwa Maisha kuwa watamuua ili kuondoa udhia, kutaifishwa shamba na mazao yake, kufyekewa migomba ya ndizi wakati ilikuwa ikimsaidia kulea wajukuu aliochiwa, vimemfanya atafute msaada kwa waandishi wa Habari ili aweze kufikisha kilio chake kwa Rais Dkt. Samia suluhu Hassan ili amsaidie.

 Baadhi ya wakulima wakilima vibarua katika shamba la Bi. Amina Msigwa aliyedai kulima na kupanda mahindi mwishoni mwa mwaka jana, lakini cha kushangaza yeye mwenyewe hajawapa ajira hiyo ya muda, bali wamepewa na watu tofauti na Bibi huyo mwenye wajukuu 19. 

Akiongea kwa hisia kali za uchungu Bi. Amina ameongeza kuwa Desemba 8,2025 alilima kwa trekta na kupanda mahindi kwenye shamba la heka 10, lakini sasa limevamiwa na watu hao hao wanalima na kumpiga marufuku kuingia katika shamba lake.

“rais mama samia, na serikali yako naomba minisaidie nyumba zangu tatu hapa shambani zimebomolewa, migomba ambayo naitegemea kulisha wanangu na wajukuu, imeng’olewa, mazao niliyopanda tangu tarehe 8.12. 2025 sasa nimenyang’ywa wanalima watu wengine, nimeuomba uongozi wa kata na Kijiji wanasaidie wamesema wao hawawezi niondoke wamenichoka”, amesema  

kwa upande wake Asha Hemed Mwagilo ambaye ni mmoja wa waliokaribishwa tangu mwaka 2012 kwa kupimiwa kiwanja cha makazi, anasema vitendo anavyofanyiwa Bi. Amina vinashangaza kwani tangu kipindi hicho hawajawahi kuyaona hayo.

"hivi ni kweli mtu anaweza kuingia shambani mwa mtu akafyeka miti, migomba na kuvamia mazao ya mtu na kuingiza watu kuanza kuyalimia huku akitoa vitisho, wakati serikali ipo inaangalia bila kutoa msaada wowote hapa kweli Rais wetu mama Samia aingilie kati", amesema

 Mwanzilishi wa kijiji cha Kang'ata kilichopo Kata ya Kang'ata wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, Said Ally Ngulati akifafanua Jambo wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu sakata la Bi. Amina Msigwa kuhusu mashamba yake.

Nae Msimamizi wa Ardhi tangu mwaka 1975, na mwanzilishi wa Kijiji hicho cha Kang’ata chenye namba 429, Said Ally Ngulati, anasema anafahamu Ardhi hiyo ni ya Amina aliyoipata toka kwa shangazi yake ambapo wakati akikabidhiwa 2009 na yeye alikuwepo.

Akiongea kwa Simu mtendaji wa Kijiji cha Kang’ata, kata ya Kang'ata wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga, Oscar Mwakilasa anasema Ofisi yao ina kazi nyingi na kwamba kama kuna mtu anayekuwa na jambo lake la kufanyiwa suluhu asubiri Foleni yake ifike.

“ni kama ilivyo mahakamani kila shauri linakuwa na tarehe na muda wake, kama mtu ana jambo lake inabidi asubiri foleni yake, tuna kazi nyingine nyingi”, amesema

Aidha Veo huyo amesema kama ni swala la Bi Amina ni la Kifamilia, inawezekana Mtendaji wa kata analijua lakini yeye halijamfikia, lakini alipoulizwa kuhusu watu waliovamia mazao ya Bi. Amina na kumtishia Maisha  asiingie tena shambani kwake, alisema “naomba kuingia kwenye ibada muda umekwisha”, akakata simu

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG