NA DENIS MLOWE ,IRINGA
SERIKALI imethibitisha kuwa ujenzi wa daraja la Isakalilo – Kitwilu, ambalo limekuwa likisubiriwa kwa zaidi ya miaka 20, utaanza kutekelezwa mara baada ya kukamilika kwa usanifu (design) uliokwishafanywa kupitia mradi wa TACTIC Awamu ya Pili.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri Ruben Kwagilwa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, wakati akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhil Fabiani Ngajilo.
Mbunge Ngajilo alitaka kufahamu lini ujenzi wa daraja hilo muhimu Linalounganisha Barabara ya Isakalilo –Kitwilu (km 3) na kusaidia kufungua njia ya kufikia Hifadhi ya Taifa ya Ruaha utaweza kuanza rasmi.
Serikali Yatamka: “Hakuna Tatizo la Fedha”
Akijibu, Naibu Waziri Kwagilwa alisema mradi huo upo katika mpango wa utekelezaji na Serikali imeweka fedha tayari kupitia bajeti ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mheshimiwa Spika, Serikali haina tatizo la fedha. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga fedha maalumu kwa ajili ya mradi wa TACTIC, na awamu ya pili ndiyo inayojumuisha ujenzi wa daraja hili pamoja na barabara za kuingia kwenye daraja,” alisema.
Alibainisha kuwa awamu ya kwanza ya mradi wa TACTIC tayari inaendelea katika Manispaa ya Iringa, ikijumuisha ujenzi wa soko la Kihesa, barabara za Mkimbizi Bima, Mtwavlla, Viziwi, na Bonetank.
Aliongeza kuwa Awamu ya Pili Kuanza utakuwa ni Daraja na Lami ya Km 3 Kuanza rasmi
Katika swali lake la nyongeza, Mbunge Ngajilo alitaka ufafanuzi kuhusu muda kamili wa kuanza kwa ujenzi na kama mapendekezo ya mmiliki wa usanifu ya kujengwa daraja lenye urefu wa mita 40 pamoja na kipande cha lami cha kilometa yatazingatiwa.
Serikali ilithibitisha kuwa ujenzi wa daraja la Isakalilo–Kitwilu utatekelezwa kulingana na usanifu huo, na kwamba utekelezaji utaanza rasmi mara tu taratibu za awamu ya pili kukamilika, ili kufungua kikamilifu njia ya kuunganisha maeneo ya Isakalilo, Kitwilu na hifadhi ya Ruaha.

