KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya Senegal, Pape Thiaw, amekataa msaada wa kifedha uliokusudiwa kumlipia faini ya dola za Marekani 100,000 aliyotozwa kufuatia tukio lililotokea baada ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2025 dhidi ya Morocco.
Baada ya adhabu hiyo kutangazwa, wananchi wa Senegal waliungana na kuanzisha kampeni maalum ya kuchanga fedha kwa lengo la kumsaidia kocha wao kulipa faini hiyo, hatua iliyoonyesha mshikamano na mapenzi makubwa waliyonayo kwa timu yao ya taifa.
Hadi sasa, kampeni hiyo imefanikiwa kukusanya zaidi ya dola za Marekani 4,300, kiasi ambacho ni sawa na takribani faranga za CFA 2,400,000, na kwa fedha ya Tanzania ni karibu shilingi milioni 10.
Mwitikio huo umeendelea kukua kila siku huku mashabiki na wadau wa soka nchini Senegal wakionyesha nia ya kuendelea kuchangia hadi kufikia lengo kamili.
Hata hivyo, Pape Thiaw ametoa shukrani zake za dhati kwa wananchi wote waliojitokeza kumuunga mkono, akieleza kuguswa sana na moyo wao wa kujali na mshikamano. Pamoja na hilo, amesisitiza kuwa hataki fedha hizo zitumike kumlipia faini yake binafsi, bali amewaomba waandaaji wa kampeni na wachangiaji waelekeze michango hiyo kwa watu wenye uhitaji mkubwa zaidi katika jamii, hususan makundi dhaifu yanayohitaji msaada wa haraka.
Hatua hiyo imeongeza heshima na pongezi kwa kocha huyo, wengi wakimtaja kama kiongozi mwenye moyo wa kujitolea na kuwajali wengine zaidi ya maslahi yake binafsi.
