BANDA MEDIA BLOG

NECTA: MAGEUZI YA ELIMU YA MSINGI YAIMARISHA UMAHIRI WA KKK

 

Na mwandishi wetu, DSM

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohammed, amesema juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, hususan katika kuimarisha stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi.

Akizungumza leo Januari 29, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa KKK kwa wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza na la pili, Profesa Mohammed amesema tukio hilo ni la kihistoria na linaonesha dhamira ya dhati ya Rais katika kuboresha elimu nchini.

Ameeleza kuwa mpango huo unawalenga watoto wenye umri wa miaka mitano hadi saba, ambao ni hatua ya msingi katika kujenga uwezo wa kujifunza. Alisisitiza kuwa mtoto asipopata stadi za KKK mapema huathirika katika nyanja zote za ukuaji ikiwemo kiakili, kijamii na kihisia.

“Mtoto anayekosa KKK ni sawa na mtoto mchanga anayekosa maziwa ya mama. Stadi hizi ndizo msingi wa elimu ya baadaye,” amesema.

Profesa Mohammed amebainisha kuwa tangu mwaka 2015 NECTA imekuwa ikifanya upimaji wa kitaifa kwa sampuli, ambapo matokeo yalionesha kuwa kati ya asilimia 67 hadi 87 ya wanafunzi walikuwa na umahiri wa KKK, huku changamoto kubwa zikiwa katika kusoma kwa ufasaha, kuandika kwa usahihi na kuhesabu.

Ameongeza kuwa mafunzo yaliyotolewa kwa walimu pamoja na maboresho ya mazingira ya ujifunzaji yamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa idadi ya wanafunzi wasio na stadi hizo.

Aidha, amesema kuwa kwa mara ya kwanza mwaka 2025 NECTA ilifanya upimaji wa kitaifa wa darasa la pili ngazi ya shule, uliowahusisha wanafunzi zaidi ya milioni 1.7 kutoka shule zaidi ya elfu 8, kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa PRN. Hatua hiyo imelenga kubaini changamoto za wanafunzi mapema ili zichukuliwe hatua stahiki kabla hawajafika madarasa ya juu.

Kuhusu ufaulu wa masomo ya sayansi na hisabati, Profesa Mohammed amesema takwimu zinaonesha kuimarika kwa matokeo, hususan katika somo la Advanced Mathematics kwa kidato cha sita, ambapo ufaulu umefikia karibu asilimia 100 katika miaka ya karibuni.

Amesisitiza kuwa wadau wa elimu wanapaswa kutumia mbinu za kisayansi kutatua changamoto zilizopo, ikiwemo kuondoa hofu ya hisabati (numerophobia) na kuboresha mbinu za ufundishaji ili kuongeza ari na ufaulu wa wanafunzi.    

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG