BANDA MEDIA BLOG

WITO WA UMOJA NA AMANI KUELEKEA KILELE CHA MIAKA 49 YA CCM, WATOLEWA IRNGA

 


NA DENIS MLOWE, IRINGA 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daud Yasin, ametoa wito kwa wanachama na wananchi kuendelea kuenzi umoja, amani na mshikamano kama nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya CCM.

Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika kata ya Ruaha ndani ya Manispaa ya Iringa, Yasin alisema kuwa kilele cha sherehe hizi kitafanyika Wilaya ya Iringa Vijijini, katika kata ya Idodi, tarehe 5 mwezi wa pili mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande.

Yasin alisisitiza kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Tumechagua Umoja na Amani kwa Maendeleo ya Taifa Letu,” akibainisha kuwa bila amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana. Alitoa rai kwa wananchi kupuuza watu wenye nia ya kuwatenganisha na kuwatia chuki ili kuchelewesha maendeleo.

Aidha, alieleza kuwa misingi ya usawa ndani ya CCM, ambayo inahimiza kutokubaguana kwa misingi ya dini, kabila au eneo, imeendelea kukijengea chama hicho imani kubwa kutoka kwa wananchi. Aliongeza kuwa imani hiyo imejidhihirisha kupitia ushindi wa madiwani katika kata 106 za mkoa huo na wabunge wote saba wa majimbo.

“Imani huzaa imani,” alisema Yasin, akibainisha kuwa wananchi wanatarajia kuona utekelezaji makini wa ilani ya CCM baada ya kukipa chama hicho ushindi mkubwa.

Ametoa maagizo kwa viongozi wa chama na serikali kuhakikisha wanawafuata wananchi, kuwasikiliza, kutatua kero zao na kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2020–2025 ambayo imeleta mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, miundombinu na mawasiliano.

“Sasa si wakati wa maneno, ni wakati wa vitendo,” alisisitiza, akitaka viongozi kuchukua hatua za kutatua changamoto badala ya kutoa majibu ya kukwepa.

  

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG