BANDA MEDIA BLOG

MAUAJI YA KAMANDA MWANDAMIZI WA M23: NI MKONO WA MAREKANI AU PAPATU YA JESHI LA KONGO? KUNA KITU YATABADILISHA?

 

YEYOTE aliyewahi tazama videos za kamatwa na ondoka ya mamluki wa Kizungu mwanzoni mwa 2025 baada ya muungano wa AFC/M23 kuteka jiji la Goma na baadae Bukavu atakumbuka sauti ya "Quick Quick" inayotoka kwa mmoja wa makamanda wa muungano huo kuwahamasisha mamluki hao kuharakisha wakati mamluki hao wakivuka mpaka wa kuingia Rwanda kwa ajili ya kusafirishwa kwa ndege kurudishwa mataifa mbalimbali walimotokea barani Ulaya. AFC/M23 iliamua kuwasamehe kwa sharti kwamba wakirejea kushirikiana na vikosi vya jeshi la Kongo (FARDC) basi watauwawa.
Sauti hiyo ya mkazo ndani ya video ni ya Luteni Kanali na Msemaji wa Muungano huo, Willy Ngoma (pichani).
Taarifa zilizothibitishwa na mamlaka za DRC lakini pia baadhi ya wanadiplomasia ni kwamba Msemaji huyo aliuawa Februari 24, 2026, majira ya saa 8:40 usiku kwa saa za DRC katika shambulizi la ndege isiyo na rubani aina ya CH-4B ya jeshi la Taifa. Willy alikuwa katika kikao- kazi na viongozi wengine sita. Shambulizi hilo, taarifa zinabaini, lilihusisha milipuko miwili- mwambatano baada ya taarifa za kijasusi ambazo FARDC ilipata kuhusu kutaniko hilo.
Willy Ngoma, ambaye baadhi ya vyanzo humtaja kwa majina ya Ngarurira Ingoma Rutikanga, alizaliwa mwaka 1974. Wakati akiuawa Febeuari 24, alikuwa na miaka 52. Ni mmoja wa viongozi muhimili wa Muungano huo; walioshuhudia mageuzi yake toka enzi za CNDP. Kama Sultani Makenga, Bertrand Bisimwa, Lautent Nkundabatwale na Bosco Ntaganda, Ngoma alipigana vita ya ukombozi Rwanda mwaka 1994 kutokea Uganda na baadae kushiriki uvamizi nchini DRC mwaka 1996 kumwondoa Mobutu Sese Seko, hata katika awamu ya pili ya vita hiyo mwaka 1998- 2003.
Ngoma na wenzake tajwa kabla ya kuwa waasi walikuwa wanajeshi katika jeshi la DRC, kama sehemu ya jitihada za utatuzi wa mgogoro huo ambao kwa muda mrefu umetajwa kuchochewa na unyanyasaji na ubaguzi wa kimfumo kwa watu wa jamii ya Kitutsi.
Kifo chake ni pigo kwa AFC/M23, kutokana na ukongwe lakini pia kipaji chake katika kuusemea kitaifa na kimataifa. Kwa upande mwingine, ni faida kwa jeshi la Taifa la DRC kutokana na muda mrefu lilivyokuwa likinyukana na vikosi vya kundi lake toka 2006 lilivyoasisiwa kwa jina la M23.
Baadhi ya wasomaji mmeniuliza, kifo hiki chaweza kuwa "kazi ya Marekani"?
Ndio na hapana yaweza kuwa majibu. Ndio, kwa sababu kwa siku za karibuni ilionesha kuchukizwa na muungano huo kutoheshimu makubaliano yaliyotiwa saini Qatar na Washington kwa kuendeleza mashambulizi katika mkoa wa Kivu Kusini. Mara kadhaa ilisisitiza vikosi vya muungano huo na washirika wake kuondoka Uvira. Licha ya kuonesha kutii, taarifa za mashambulizi ziliendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Imekuwa pia ikionesha kutoridhishwa na Rwanda kuendelea kuunga mkono harakati zao.
Marekani kwa uwezo wake kijasusi na kijeshi, si ajabu akawa 'amesaidia' katika shambulizi hilo. Kwa upande mwingine, jibu la hapana linaweza kuwa sahihi kutokana na kwamba yamkini FARDC yenyewe katika jitihada zake ikawa tu ilifanikiwa kunasa taarifa za kijasusi na kuzifanyia kazi kwa wakati.
Je, M23 itatetereka?
Licha ya kurasa zao kuonesha kauli za majigambo tangu kuripotiwa mauaji hayo, ukweli ni kwamba kwa kiasi mauaji haya yatawayumbisha. Willy hakuwa mpiganaji wa kawaida. Alikuwa KIONGOZI MWANDAMIZI, MTU MWENYE USHAWISHI, KIPAJI CHA PEKEE KATIKA KUFANYA PROPAGANDA na MWANACHAMA KINDAKINDAKI. Alilijua kundi vizuri. Alilitetea kwa wivu na upendo usiomithilika. Alilipenda. Alijitoa kwake kwa hali na mali. Alivaa uhusika wa M23 usiku na mchana. Alikuwa zaidi ya mfuasi.
Ni kichekesho kusema kwamba kifo chake hakina ombwe au madhara ndani ya muungano huo.
Kwa mtazamo wa propaganda, ni sahihi kabisa kwa kile AFC/M23 wanachofanya katika kurasa zao kuionesha dunia kwamba hakijawaathiri; kwamba wako imara bila kuyumba. Hata hivyo, sicho kilicho mioyoni. Kihisia na kifikra wana mshtuko. Wana uchungu na hasira. Yamkini pia wakawa na uoga, hasa kwa kuzingatia kwamba shambulizi hilo lilifanywa katika mazingira ya "ambush" au "tit- for- tat."
Inawezekana hata viongozi wake wakaanza kuwa makini zaidi katika mizunguko yao. Pengine wakapunguza hata mizunguko kwa siku za karibuni. Pengine ikachagiza utekelezaji wa makubaliano ya Washington na hata Qatar kwa haraka na karibuni kuliko ilivyoonekana awali.
Kuna uwezekano pia wa mauaji hayo kuzaa mashambulizi ya kisasi, yatakayoumiza zaidi raia wa kawaida. Pengine mlipuko wa vita baina ya AFC/M23 na majeshi ya FARDC na washirika wao ukazuka upya. Kuna mengine ambayo yanaweza kujitokeza.
Kwa msukumo wa uhitaji wa Marekani katika sekta ya madini iliyodhibitiwa na Urusi na China muda mrefu nchini humo, tunaweza kushuhudia pia ongezeko la miito na shinikizo kuweka silaha chini ili kuepusha mauaji kama haya zaidi kwa pande zote.
Asili ya Willy Ngoma huripotiwa kwa kukinzana.
Wakati mwenyewe mara zote alijitaja kama Mkongomani anayezungumza Kinyarwanda au Mnyamulenge kutoka mkoa wa Kivu Kaskazini nchini DRC, vyanzo vingine hupinga kwa kumtaja kama mzaliwa wa Kinigi nchini Rwanda. Ngoma amekuwa katika orodha ya viongozi wa muungano huo waliowekewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa kwa muda mrefu kutokana na kile kinachoitwa "ushiriki katika mauaji ya raia wasio na hatia" kwa muda mrefu kupitia mashambulizi yanayoendeshwa mara kwa mara na kundi lake.
Mara zote alitetea hatua za kijeshi zilizochukuliwa na kundi hilo kwa kudai kwamba jamii yake ya Banyamulenge imekuwa muhanga mkubwa wa matendo zaidi ya hayo hivyo ni haki na wajibu wao kuilinda na kujilinda kwa"namna yoyote inayowezekana."
Wakosoaji wa harakati za M23 wanaamini kwamba kifo chake ni ukumbusho kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haiwezi kamwe "kujisalimisha" kwa wanaotaka kuigawa.
Hadi sasa, AFC/M23 haijatoa msimamo wowote juu ya nini watafanya baada ya tukio hilo. Baadhi ya raia wa mkoa wa Mashariki wanaonekana kutiwa hofu na ukimya huo, wakiona kwamba yamkini ukawa wa hatari ya mashambulizi au unyama kama njia ya kutuliza hasira yao. Miezi michache iliyopita muungano huo ulipata wapiganaji wapya zaidi ya 4000 baada ya kuhitimu mafunzo.
Kwa namna gani kifo hiki kinaweza kuwa na matokeo chanya au hasi, ni suala la kungoja na kuona.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG