
Serikali imewahakikishia wananchi kuwa hakuna uhaba wa mafuta nchini, ikieleza kuwa akiba iliyopo pamoja na inayoendelea kuwasili inatosheleza mahitaji kwa kipindi cha miezi miwili hadi mitatu.
Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, amesema hali ya upatikanaji wa mafuta ni shwari, huku Serikali ikiendelea kufuatilia mwenendo wa soko la dunia kutokana na vita vinavyoendelea katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
“Mafuta yaliyopo nchini kwenye matenki, Petrol tuna lita 95,256,342; mafuta ya petrol yaliyowasili nchini ni lita 1,466,337; mafuta yaliyopo njiani kwenye meli ni lita 138,737,332. Hivyo, jumla ya mafuta ya Petrol yatakayokuwepo ni lita 380,677,011, na yanatosha kwa matumizi ya siku 61,” amesema Dkt. Mataragio.
Ameongeza kuwa kuna mikataba ya mafuta iliyoingiwa na mzabuni yenye jumla ya lita 183,500,450 ambayo yatafika nchini mwezi wa nne, hivyo kufanya jumla ya mafuta ya Petrol yaliyopo kwenye matenki, yatakayowasili kwa meli pamoja na yaliyopo kwenye mikataba kufikia lita 563,682,461, kiasi kinachotosheleza kwa siku 91.
Kwa upande wa mafuta ya Diesel, Dkt. Mataragio amesema mafuta yaliyopo kwenye matenki ni lita 55,744,397; yaliyowasili nchini ni lita 122,893,285; na yaliyopo njiani kwenye meli ni lita 184,662,480. Hivyo, jumla ya mafuta ya Diesel ni lita 362,433,845, yanayotosha kwa matumizi ya siku 44.
Amefafanua kuwa mafuta ya Diesel yaliyopo kwenye mikataba na wabuni ni lita 167,321,343, na kufanya jumla ya mafuta yote ya Diesel yaliyopo nchini, yanayokuja kwa meli na yaliyopo kwenye mikataba kufikia lita 530,621,505, kiasi kitakachotosheleza kwa siku 64.
Kwa upande wa mafuta ya ndege, amesema yaliyopo kwenye matenki ni lita 35,241,028 na yaliyopo kwenye mikataba ni lita 23,779,725, hivyo kufanya jumla ya lita 59,020,753 zitakazotosheleza kwa siku 97.
Hata hivyo, ameonya kuwa kutokana na kuendelea kwa vita katika Mashariki ya Kati, kuna uwezekano wa ongezeko la bei za mafuta kutokana na kupanda kwa bei katika soko la dunia.
