Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema makampuni ya teknolojia hayapaswi kushawishi matakwa ya serikali yake na ya nchi nyingine za Umoja wa Ulaya kuhusu kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana wa chini ya mika 16.
"Na hawatatuvunja moyo wala kutuvuruga, kwa sababu sauti zetu zenye mantiki, sauti za walio wengi na za demokrasia ni wazi hazitashawishiwa na watu wanaomiliki teknolojia na waliobobea katika mfumo huu, " alisema Sanchez.
Wataalamu wanasema kwa Watoto kutumia muda mwingi kuvinjari maudhui yenye madhara yanasababisha akili za vijana kujijenga upya hali inayosababisha vijana hao kukumbwa na wasiwasi Pamoja na hatari zingine za kiafya, na ndio sababu serikali za nchi za Ulaya zinalazimika kuchukua hatua.
Paul O. Richter, Mtalaamu mshirika katika jopo la watoa ushauri katika shirika la Bruegel lenye makao yake makuu mjini Brussels, ameiambia DW kwamba utafiti mwingi unaonyesha uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya mitandao ya kijamii na masuala ya afya ya akili.
Umoja wa Ulaya waunga mkono hatua hizo
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen pia ameelezea kuunga mkono ukomo wa umri katika Jumuiya ya Umoja ya Ulaya yote kuambatana na sheria mpya ya Australia ambayo imeweka kikomo cha umri wa miaka 16 ndipo mtoto atakaporuhusiwa kuanza kutumia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo baadhi ya wataalamu wanahoji jinsi marufuku kama hiyo itakavyotekelezwa na kama kweli itafanya kazi. Wakati huo huo, sheria kuu ya kidijitali ya Umoja wa Ulaya inaonekana kudhoofika katika kuendesha mabadiliko ya kimfumo kwenye majukwaa makubwa ya mtandaoni.
Wakati huo huo, wabunge wa Ulaya mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita walipendekeza kuwekwe marufuku ya mitandao ya kijamii kote barani Ulaya kwa watoto walio chini ya miaka 16, huku pia wakipendekeza kwamba watoto wa miaka 13 hadi 16 wanaweza kupewa ruhusa ya kutumia mtandao huo lakini kwa idhini ya wazazi wao.
Mjadala wapamba moto
Wazo mojawapo linalojadiliwa ni juu ya namna ya kuthibitisha umri ambapo imependekezwa kuanzishwa kitambulisho cha kidijitali katika nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya. Mtalaamu mshirika katika jopo la watoa ushauri wa shirika la Bruegel Paul O. Richter, amesema kitambulisho cha kidijitali kitakuwa ndio chombo ambacho kitathibitisha umri wa mtumiaji bila kuathiri maelezo yake binafsi.
Kwa upande wake Marc Damie, msemaji wa jukwaa linaloendesha za haki za kiteknolojia na haki za kidijitali nchini Ufaransa linaloongozwa na vijana amedai kwamba maelezo kuhusu programu au vitambulisho vya kuthibitisha umri hayako wazi na kwamba marufuku hiyo itasababisha matatizo. Amesema hatua hiyo ni kipimo cha mfano tu kwa upande wa wanasiasa lakini si suluhisho halisi.
Damie amesema ni wakati muafaka kwa nchi za wanacham wa Umoja wa Ulaya kuwekeza kwa pamoja katika njia mbadala badala ya kutegemea majukwaa ya mitandao ya kijamii yasiyo ya Ulaya . Ameongeza kusema kuwa bila ya nchi za Ulaya kujikomboa zitaenedelea kuwa mateka wa makampuni makubwa ya Marekani.




