Na Maiko Luoga Dodoma
Katibu Mkuu, Kanisa Anglikana Tanzania, Kasisi Canon. Dkt. George Otieno Lawi, ameelekeza, Idara ya Utume na Uinjilisti, Kanisa Anglikana Tanzania kufanya kazi kwa Bidii ili kuongeza kasi ya upandaji Makanisa.
Katibu Mkuu Lawi ametoa maagizo hayo, wakati akizungumza na wajumbe wa Kikao cha Kamati Tendaji ya Utume na Uinjilisti na Waratibu wa Kanda za Kanisa Anglikana Tanzania, kilichofanyika 25 machi 2026.
“Idara ya Utume na Uinjilisti mnao wajibu wa kufanya kazi ya Uinjilishaji na kuchochea kasi ya upandaji makanisa nchini, ili katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Kanisa likue kwa kasi” alisema Katibu Mkuu Lawi.
Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi Kuu za Kanisa Anglikana Tanzania Dodoma, chini ya Mwenyekiti Lay Canon. Nicholaus Mgaya na Katibu Kasisi Canon. Linus Buriani, Mratibu wa Utume na Uinjilisti KAT, kwa lengo la kupitisha mpango kazi wa Mwaka 2026.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kikao hicho, Lay Canon. Nicholaus Mgaya alisema, Idara imepokea na kufanyia kazi ushauri na maagizo ya Katibu Mkuu ili kuongeza kasi ya kutangaza Injili ya Kristo.
Wajumbe walipata nafasi ya kuona mradi wa jengo la kitega uchumi cha Kanisa Anglikana Tanzania, lenye gorofa tano, na kwamba 21 juni 2026 itafanyika harambee ya kuchangia zaidi ya bilioni 1.5 ili kukamilisha mradi huo.

