
NA DENIS MLOWE IRINGA
JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limevunja mtandao mkubwa wa wizi wa pikipiki unaofanya kazi katika mikoa kadhaa nchini, baada ya kukamata pikipiki 115, watuhumiwa tisa na mali mbalimbali zinazodaiwa kupatikana kwa njia ya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Allan Bukumbi, alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na operesheni maalum iliyofanyika tarehe 17 Januari 2026 katika eneo la Kihesa, Manispaa ya Iringa.
“Kupitia operesheni hii tumefanikiwa kubaini mtandao mpana uliokuwa ukijihusisha na wizi wa pikipiki katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro na maeneo mengine. Haya ni mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya uhalifu,” alisema Bukumbi.
Katika operesheni hiyo ya awali, watuhumiwa watatu Ernest Mgaya, Oscar Malinda na Emilio Mfilinge walikamatwa wakiwa na pikipiki tatu zinazodaiwa kuibwa mkoani Dodoma.
Baada ya mahojiano, walikiri kuiba zaidi ya pikipiki 50 kila mmoja na kutengeneza kadi bandia zilizokuwa zikiuzwa kwa washirika wao wa Makambako.
Uchunguzi uliendelea hadi katika mji wa
Makambako, ambako Polisi waliwakamata watuhumiwa wengine wawili, James Mgaya (29) na Jackson Chaula (28), wanaodaiwa kuwa wanunuzi wakuu wa pikipiki hizo. Katika upekuzi, pikipiki 82, guta moja, vibao 19 vipya vya namba za usajili, kadi bandia 50 za pikipiki, mashine ya kuoshea magari na kiasi cha shilingi 6,430,000/= vilipatikana.
Kamanda Bukumbi alisema mtandao huo pia unahusisha watu wanaotoa fedha kwa ajili ya kufanikisha wizi katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya na Arusha.
“Tunatoa wito kwa wananchi wote walioibiwa pikipiki kujitokeza katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Iringa kwa ajili ya utambuzi. Operesheni bado inaendelea,” aliongeza Bukumbi.
Kwa ujumla, mali zilizokamatwa ni pikipiki 115, watuhumiwa tisa, gari moja, bajaj moja, guta moja, mashine ya kuoshea magari na vifaa mbalimbali vinavyohusishwa na uhalifu huo.

Tags
POLISI